
Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Nestory John kutoka Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ameitaka jamii kujenga utamaduni wa kutembelea na kusaidia makundi yenye mahitaji maalum.
Hayo amezungumza Novemba 20, 2026 alipowaongoza Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Polisi Mkoani humo kuwatembelea Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwenge wenye matatizo ya afya ya akili na usonji.
SSP Nestory John amesema, Jeshi la Polisi kupitia chama cha ushirika cha URA SACCOS wameguswa na changamoto walizonazo watoto hao na kuona umuhimu wa kusaidia mahitaji mbalimbali ikiwemo vyakula, magodoro na sare za Shule.
Naye, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bi.Annes Mwakaje amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kuichagua Shule hiyo na kupata nafasi ya kuitembelea na kutoa mahitaji mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia watoto.
Aidha, Mwalimu Mwakaje ameiomba jamii kutowatenga watoto wenye matatizo ya afya ya akili na usonji huku akisisitiza kuwa watoto hao wana haki ya kupata elimu pamoja na haki nyingine za msingi kama watoto wengine hivyo wasiwafiche bali wawapeleke Shule.
Kwa upande wake, Meneja wa URA SACCOS tawi la Mbeya Mrakibu wa Polisi (SP) Liberatus Rutariba amesema kuwa, kuelekea maadhimisho ya miaka 20 ya URA SACCOS tangu kuanzishwa wamekuwa wakitembelea makundi mbalimbali ya jamii na kutoa msaada wa vitu ikiwa ni sehemu ya kuthamini mchango wa jamii na kurejesha kwa jamii (Corporate Social Responsibility).
