Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
SERIKALI imeweka mkakati wa kukuza uzalishaji wa dawa za tiba asili viwandani kwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini, hatua inayolenga kuongeza thamani ya rasilimali za ndani, kuunda ajira na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa za afya barani Afrika.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema hayo leo Novemba19,2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Dhifa ya Uwekezaji katika Dawa za Tiba Asili (Asili Investment Gala 2027), inayotarajiwa kufanyika Aprili 2026.
Amesema kupitia uwekezaji huo, Serikali inalenga kuimarisha tafiti, ubunifu na ujenzi wa viwanda vitakavyozalisha dawa za tiba asili kwa kutumia mimea tiba na malighafi nyingine zinazopatikana nchini.
Amesema hatua hiyo itafungua fursa za kiuchumi katika mnyororo mzima wa uzalishaji, kuanzia kilimo cha mimea tiba, ukusanyaji wa malighafi, uchakataji wa kisasa hadi uzalishaji wa dawa, hivyo kuongeza ajira kwa vijana na pato la Taifa.
Mchengerwa amesema ili kufanikisha azma hiyo, Serikali imeandaa dhifa hiyo itakayokutanisha washiriki zaidi ya 1,000 kutoka sekta binafsi, taasisi za fedha, jumuiya ya kidiplomasia, washirika wa maendeleo na taasisi za utafiti kwa ajili ya kuhamasisha uwekezaji.
Amesema uwekezaji huo pia utasaidia kuimarisha uwezo wa kitaifa katika kufanya tafiti za kisayansi na kuthibitisha usalama, ubora na ufanisi wa dawa za tiba asili kabla ya kuruhusiwa kutumika katika huduma za afya.
Amebainisha kuwa Serikali inalenga ifikapo mwaka 2030 kuhakikisha tiba asili inajumuishwa katika mfumo rasmi wa huduma za afya nchini, ikiwemo kuangalia uwezekano wa huduma hizo kujumuishwa katika mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote.
Amesema zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanatumia tiba asili, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mifumo rasmi ya udhibiti na kuimarisha ushirikiano na wadau ili kuhakikisha dawa zinazozalishwa zinakidhi viwango vya usalama na ufanisi.
Ametoa wito kwa wafanyabiashara, kampuni binafsi, taasisi za fedha, wamiliki wa migodi na mashirika ya Serikali kushiriki katika dhifa hiyo kwa kuwekeza katika sekta hiyo, akisisitiza kuwa Serikali itasimamia michango itakayopokelewa kupitia akaunti rasmi na kuhakikisha inatumika kwa shughuli zilizoidhinishwa.


