Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha madini yanayozalishwa nchini yanaongezewa thamani ndani ya nchi ili kukuza uchumi wa viwanda, kuongeza ajira, kuimarisha mapato ya Taifa na kuhakikisha wananchi wananufaika zaidi na rasilimali hizo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Hayo yameelezwa Novemba 19, 2026 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati akifungua Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania (TMIC 2026), jijini Dar es Salaam.
Amesema Tanzania imejielekeza katika kuimarisha viwanda vya ndani vya uchenjuaji, usafishaji, uyeyushaji na utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na madini ili kupunguza utegemezi wa kuuza nje madini ghafi na kuongeza manufaa ya rasilimali hizo kwa uchumi wa Taifa.
Amesema nchi nyingi za Afrika bado hazijanufaika kikamilifu na utajiri wa rasilimali madini kutokana na uhaba wa viwanda vya kuongeza thamani, hivyo Tanzania imeendelea kuboresha sera, sheria na kanuni ili kuvutia uwekezaji na kuunganisha sekta ya madini na sekta nyingine muhimu zikiwemo viwanda, nishati na kilimo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Ndejembi amesema Serikali imeridhia kutenga asilimia 10 ya mapato yatokanayo na madini kwa ajili ya kufadhili utafiti wa rasilimali mpya kupitia Mfuko wa Utafiti wa Madini (Minerals Survey Fund), huku akiielekeza Wizara ya Madini kuhakikisha fedha hizo zinasimamiwa vizuri na kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
Aidha, ameitaka Wizara ya Madini kuhakikisha wawekezaji wanatekeleza kwa wakati masharti ya leseni walizopewa na kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo, ambao wanachangia zaidi ya asilimia 40 ya mapato yatokanayo na shughuli za madini.
Katika kutambua mchango wake katika kuimarisha usimamizi, mageuzi na maendeleo ya sekta ya madini nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa tuzo maalum ya kutambua uongozi wake na jitihada zake za kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuongeza thamani ya madini na kuhakikisha rasilimali hizo zinachangia ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi wa wananchi.
Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa ajenda ya kuongeza thamani ya madini, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema sekta hiyo imeendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Taifa kwa kuchangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa, huku mauzo ya madini nje ya nchi yakifikia Dola za Marekani bilioni 5.4, sawa na zaidi ya shilingi trilioni 13.
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha uwekezaji katika viwanda vya kuongeza thamani ya madini, ikiwemo viwanda vinane vya kusafisha dhahabu na viwanda 16 vinavyoendelea kujengwa kwa ajili ya kuchakata madini ya kimkakati, yakiwemo nikeli na shaba, pamoja na miradi ya uchakataji wa madini ya tembo na Ferro-Niobium.
Kuhusu uimarishaji wa akiba ya Taifa, Mavunde amesema Tanzania imefanikiwa kukusanya akiba ya dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inayofikia tani 39.6, hatua inayoifanya nchi kuingia miongoni mwa mataifa matano ya Afrika yenye akiba kubwa ya dhahabu kupitia benki kuu zao.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini kupitia ajira, utoaji wa bidhaa na huduma, pamoja na fursa za uwekezaji katika mnyororo mzima wa thamani wa madini.
Akizungumzia mkutano huo, Waziri Mavunde amesema TMIC 2026 umekutanisha washiriki zaidi ya 1,715 kutoka ndani na nje ya nchi, ukiwa jukwaa muhimu la kuimarisha diplomasia ya uchumi, kuvutia uwekezaji na kujadili fursa mbalimbali za kuongeza thamani ya madini nchini.
Mkutano huo unafanyika kuanzia Novemba 19 hadi 21, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, ukiwa na kaulimbiu isemayo: “Madini Yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi.”

