📍 Dodoma
WAKALA wa Vipimo (WMA) imeimarisha utoaji wa elimu kwa maafisa usafirishaji maarufu kama bodaboda kuhusu matumizi ya vipimo sahihi, ili kuwajengea uwezo wa kulinda haki za wananchi wanaponunua bidhaa mbalimbali zikiwemo gesi za kupikia, nyama na bidhaa zinazouzwa kwa uzito katika masoko.
Elimu hiyo inalenga kuwafanya maafisa hao kuwa mabalozi wa matumizi sahihi ya vipimo katika jamii, kutokana na nafasi yao muhimu ya kuunganisha wafanyabiashara na wateja, hususan familia zinazowategemea kuwasilisha bidhaa majumbani.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu hiyo Novemba 17,2026 jijini Dodoma, Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dodoma, Edward Patrick, amesema maafisa usafirishaji ni wadau muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa zenye uzito na ujazo unaolingana na malipo wanayofanya.
Amesema kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wananchi kutopata kiwango sahihi cha bidhaa wanazonunua kutokana na kutokuzingatia taratibu za upimaji, hali inayochangia malalamiko ya kupunguziwa gesi za kupikia, nyama na bidhaa nyingine.
“Familia inapomtuma bodaboda kununua mtungi wa gesi, ni muhimu kuhakikisha mtungi huo unapimwa kabla ya kulipiwa na kusafirishwa kwenda nyumbani, ili kuthibitisha kuwa kiasi cha gesi kilichomo kinalingana na kiwango kinachotakiwa.”amesema Bw.Patrick
Amesema hatua hiyo itawasaidia wananchi kuwa na uhakika wa bidhaa wanazonunua, huku maafisa usafirishaji wakipata uwezo wa kujibu malalamiko ya wateja wao kwa kuwa mashahidi wa upimaji uliofanyika wakati wa manunuzi.
“Maafisa hao wanapaswa kuwa makini wanapotumwa kununua nyama katika mabucha, kwa kuhakikisha wanashuhudia bidhaa ikipimwa na kuthibitisha uzito wake badala ya kuagiza kwa njia ya simu bila kujiridhisha na kiwango wanachonunua.”amesisitiza
Ameongeza kuwa mizani inayotumika kufanya biashara inapaswa kuwa imehakikiwa na Wakala wa Vipimo, ikiwa na stika inayoonesha uhalali wa matumizi yake, huku mtumiaji akihakikisha mizani imekaa vizuri na iko katika hali sahihi kabla ya kuanza kupima bidhaa.
Katika hatua nyingine, Patrick amesema bidhaa zinazouzwa katika masoko, ikiwemo viazi na bidhaa nyingine za kilimo, zinapaswa kuuzwa kwa uzito kwa mujibu wa matakwa ya sheria inayosimamiwa na Wakala ili kuondoa mianya ya udanganyifu na kuhakikisha mnunuzi na muuzaji wanapata haki zao.
Amesema Wakala imeamua kutumia makundi yanayokutana na wananchi kila siku, yakiwemo maafisa usafirishaji, kama njia mojawapo ya kufikisha elimu hiyo hadi majumbani, ambako wananchi wengi hununua bidhaa kupitia watu wanaowatumia kufanya manunuzi.
Ameongeza kuwa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dodoma imeanzisha klabu za vipimo katika shule, kwa lengo la kuwajengea watoto uelewa tangu wakiwa wadogo na kuwafanya kuwa mabalozi wa matumizi sahihi ya vipimo katika familia na jamii kwa ujumla.
Amesema mpango huo unaenda sambamba na utoaji wa elimu kwa madiwani, ambao wanatarajiwa kutumia mikutano yao na wananchi kufikisha ujumbe kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi na namna ya kutambua mizani inayokidhi matakwa ya kisheria.
Kuhusu hatua zinazochukuliwa dhidi ya wafanyabiashara wanaokiuka sheria za vipimo, Patrick amesema Wakala inaendelea kutoa elimu na kuchukua hatua za kisheria kwa wale wanaobainika kutumia mizani au vifaa vingine vya kupimia ambavyo havijahakikiwa.
Patrick amesema matumizi ya vipimo sahihi ni sehemu muhimu ya kujenga uchumi imara wa familia na taifa, hivyo kila mdau anapaswa kutimiza wajibu wake katika kuhakikisha bidhaa zinazonunuliwa na kuuzwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa.
Amesisitiza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya maandalizi ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambayo yanahitaji jamii yenye uelewa, uwajibikaji na matumizi sahihi ya vipimo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo (WMA), Francis Olwero, amewataka maafisa usafirishaji kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi wanaponunua bidhaa kwa niaba ya wateja wao, ili kuepusha udanganyifu na kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa kulingana na kiasi walicholipia.
Amesema maafisa hao ni wadau muhimu wa WMA kutokana na jukumu lao la kuwafikishia wananchi bidhaa mbalimbali majumbani, hivyo wanapaswa kuwa na uelewa wa namna ya kuhakiki bidhaa wanazonunua, ikiwemo gesi za kupikia na nyama, kabla ya kuzisafirisha kwa wateja.
Aidha, amewahimiza maafisa hao kuwa mabalozi wa kueneza elimu ya vipimo sahihi kwa wenzao na jamii kwa ujumla, ili kuongeza uelewa na kupunguza malalamiko yanayotokana na bidhaa kupunguzwa.
Naye Mwenyekiti wa Maafisa Usafirishaji Mkoa wa Dodoma, Baraka Obadia Ngue, amewataka maafisa usafirishaji nchini kuzingatia taratibu za vipimo sahihi wanapotekeleza maagizo ya wateja ya kununua bidhaa mbalimbali, ili kulinda uaminifu na kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza kati yao na walaji.
Amesema maafisa hao wana wajibu wa kuhakikisha bidhaa wanazonunua kwa niaba ya wateja, ikiwemo gesi za kupikia, nyama, vyakula na nafaka, zinakuwa na uzito unaolingana na kiwango kilichoelekezwa.
Ngue amesema mafunzo hayo yamewajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kushirikiana na wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa zinapimwa kwa usahihi kabla ya kuzisafirisha kwa wateja.
Amesema maafisa usafirishaji wanapaswa kuomba bidhaa zipimwe na kujiridhisha kuwa kiasi kilichonunuliwa kinalingana na oda ya mteja, badala ya kuchukua bidhaa bila kuthibitisha uzito wake.
Amesisitiza kuwa katika ununuzi wa bidhaa kama gesi na nyama, ni muhimu kuhakikisha mizani inayotumika imehakikiwa na WMA na ina stika halali inayoonesha kuwa imekaguliwa na kukidhi matakwa ya kisheria.
Aidha, Ngue ametoa wito kwa maafisa usafirishaji wa mikoa yote nchini kutumia elimu waliyoipata kuhakikisha wanakuwa waaminifu katika huduma zao, akibainisha kuwa wanaponunua bidhaa zenye vipimo pungufu bila kujiridhisha, wanaweza kulaumiwa na wateja wao kwa makosa ambayo huenda yamesababishwa na wafanyabiashara.

