Na Mwandishi Wetu-CHINA
Tume ya Ushindani (FCC) imetumia Maonesho ya Tisa ya Kimataifa ya Uagizaji wa Bidhaa China (CIIE), yaliyofanyika jijini Shanghai, nchini China, kuitangaza Tanzania kama eneo salama, lenye ushindani wa haki na fursa nzuri za biashara na uwekezaji kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Ushiriki wa FCC katika maonesho hayo yaliyofanyika kuanzia Novemba 5 hadi 12, 2026, ulikuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha taswira ya Tanzania katika soko la kimataifa, kwa kuonesha mifumo ya udhibiti inayolenga kujenga mazingira bora ya biashara, kulinda maslahi ya walaji na kuhakikisha wafanyabiashara wanashindana kwa usawa.
Ujumbe wa Tanzania ulioshirikisha taasisi za Serikali na sekta binafsi uliongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, ambaye kupitia maonesho hayo alieleza mchango wa taasisi hiyo katika kusimamia ushindani wa haki, kuzuia vitendo vinavyoweza kupotosha soko na kulinda walaji dhidi ya mienendo isiyo ya kiushindani.
Kupitia banda la Tanzania, FCC ilipata fursa ya kuwafahamisha wadau wa kimataifa kuhusu wajibu wake katika kuhakikisha shughuli za kibiashara zinaendeshwa kwa uwazi na haki, hatua inayochangia kujenga mazingira yanayovutia mitaji, kukuza biashara na kuongeza imani ya wawekezaji wanaotaka kuingia katika soko la Tanzania.
Katika maonesho hayo, banda la Tanzania lilitembelewa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban, ambaye alipokelewa na Bi. Ngasongwa na kupongeza juhudi za FCC katika kulinda ushindani wa soko na kuitangaza Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.
Mhe.Shaaban alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za Serikali na sekta binafsi katika kuvutia wawekezaji, kupanua wigo wa biashara na kuendeleza mahusiano ya kiuchumi na kibiashara kati ya Tanzania na China.
Ushiriki wa FCC katika CIIE unadhihirisha umuhimu wa taasisi za udhibiti katika kujenga mazingira wezeshi ya uwekezaji, kwa kuwa pamoja na fursa za masoko na biashara, wawekezaji huzingatia pia uwepo wa mifumo madhubuti inayolinda ushindani na kuhakikisha shughuli za kiuchumi zinafanyika kwa uwazi.
Hatua hiyo inatarajiwa kuchangia kuongeza uelewa wa jumuiya ya kimataifa kuhusu fursa zilizopo Tanzania, kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kuvutia uwekezaji wenye tija, huku FCC ikiendelea kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha soko linaendeshwa kwa misingi ya ushindani wa haki na ulinzi wa walaji.


