Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe, John Kahyoza akizungumzia matumizi ya Mahakama Mtandao ofisini kwake jana
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe, Zephrine Galeba ya akiendesha shauri kwa njia ya Mahakama Mtandao katika ukumbi wa Mahakama hiyo jana.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Mhe.Rahim Mushi akisikiliza shauri kwa njia hiyo.
Picha na Francisca Swai –Mahakama Kuu Musoma.
…………………………………………………………
Na. Francisca Swai- Mahakama Kuu Musoma
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, imesikiliza jumla ya mashauri kumi 18 kwa njia ya Mahakama Mtandao ‘Video Conference’ tangu ilipoanza kutumia teknolojia hiyo Mei 5, mwaka huu.
Akizungumzia matumizi ya Mahakama Mtandao, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe, John Kahyoza alisema walianza kusikiliza mashauri mawili yote yakiwa yanayohusu maombi ya kukata rufaa nje ya muda yalisikilizwa mbele yake wakati wafungwa wakiwa katika gereza la Musoma bila ya wao kufika Mahakamani.
Jaji Kahyoza alifafanua kuwa mashauri 10 yalisikilizwa mbele yake, manne yalisikilizwa na Mhe, Jaji, Zephrine Galeba na mashauri yaliyobakia yalisikilizwa na Mhe, Jaji Ephery Kisanya.
‘‘Mahakama ya Tanzania ilianza kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao muda mrefu katika baadhi ya Mahakama nchini ikiwa ni katika kutekeleza mpango mkakati wake wa miaka mitano (2015/2016 – 2019/2020). Hata hivyo jitihada hizo zimetiliwa mkazo kama njia ya kuepuka kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha homa ya mapafu (COVID 19)”, alisema Jaji Kahyoza.
Aliongeza kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma pia imeanza kusikiliza mashauri kwa njia hiyo Mei 12, mwaka huu, ambapo mashauri matatu yalisikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe, Rahim Mushi na kuaihirishwa bila ya Wakili wa Serikali Mhe, Jesse Temba na washtakiwa kufika mahakamani hapo.
Jaji Kahyoza alisisitiza kwamba Mahakama hiyo, itaendelea kusikiliza mashauri kwa mtandao. Pia itawekeana ratiba maalumu na Mahakama ya Hakimu Mkazi, zikiwemo za Wilaya ili kutekeleza maagizo ya viongozi wa juu wa Mahakama wakiwemo viongozi wa kitaifa wanaosisistiza kuepuka msongamano na mikusanyiko hasa katika kipindi hiki cha janga la Corona.