Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

TANZANIA imeongeza kasi ya kuvutia uwekezaji wa kimkakati katika sekta ya madini, huku Serikali ikisaini mikataba ya makubaliano na kampuni 14 za ubia kwa ajili ya kuendeleza miradi ya madini ya kimkakati, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji, uchakataji na thamani ya rasilimali hizo nchini.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha madini yanayozalishwa nchini yanaongezwa thamani kabla ya kuuzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi, sambamba na kukuza viwanda, kuongeza ajira na mapato ya Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Novemba 17, 2026, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema mikataba hiyo inahusu miradi ya madini ya kinywee, nikeli, niobium, madini adimu ya ardhini (REE) na gesi ya helium.

Amesema mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali yameendelea kuchochea maendeleo ya sekta hiyo, ambapo mchango wake katika Pato la Taifa umeongezeka hadi asilimia 10.3 mwaka 2025 kutoka asilimia 7.8 mwaka 2024.

Mavunde amesema zuio la kusafirisha madini ghafi nje ya nchi limechangia kuongezeka kwa viwanda vya uongezaji thamani, ambapo kwa sasa Tanzania ina viwanda nane vya kusafisha dhahabu na viwanda 16 vya uchakataji wa madini ya shaba viko katika hatua ya ujenzi, vikiwemo tisa vinavyojengwa Dodoma.

Amesema pia Kilwa kimezinduliwa kiwanda kikubwa cha madini ya chumvi chini ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), huku Songwe kukijengwa kiwanda cha nne duniani cha kuyeyusha na kuchakata madini ya niobium.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi imeongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 4.12 mwaka 2024 hadi Dola bilioni 5.40 mwaka 2025, huku mapato ya Serikali yakipanda kutoka Sh bilioni 526 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi Sh trilioni 1.39 mwaka wa fedha 2025/2026.

Aidha, amesema ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka kwa wazawa katika sekta ya madini umeongezeka kutoka Sh bilioni 884.09 mwaka 2010 hadi Sh trilioni 5.2 mwaka 2025, hali inayoonesha kuimarika kwa ushiriki wa Watanzania katika shughuli za sekta hiyo.

Amesema hadi Aprili 2025, sekta ya madini ilikuwa imetoa ajira rasmi 19,874, ambapo asilimia 97.4 zilikuwa za Watanzania, huku wachimbaji wadogo wakichangia takribani asilimia 40 ya uzalishaji wa madini nchini.

Mavunde amesema Serikali imeendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kupitia upatikanaji wa masoko, vifaa, teknolojia na mitaji, ikiwemo mikopo kupitia benki na taarifa za kijiosayansi zitakazosaidia kuboresha shughuli zao.

Katika hatua nyingine, amesema kwa mara ya kwanza Tanzania imetunga sheria inayotenga asilimia 10 ya mapato ya kila mwaka yatokanayo na sekta ya madini kwa ajili ya kugharamia shughuli za utafiti wa madini, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa taarifa za rasilimali zilizopo nchini.

Akizungumzia Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC 2026), amesema unatarajiwa kufanyika Novemba 19 hadi 21, mwaka huu, ukitarajiwa kuhudhuriwa na washiriki 1,715, wakiwemo 226 kutoka nje ya nchi.

Amesema mkutano huo wenye kaulimbiu ya ‘Madini Yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi’ utafunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku ukihusisha Mawaziri wa Madini kutoka mataifa mbalimbali na watoa mada zaidi ya 57 kutoka Afrika, Ulaya, Asia na Marekani.

Ameeleza kuwa mkutano huo utakuwa na vikao vya Mawaziri wa Madini, mikutano ya kibiashara kati ya kampuni, mafunzo ya uongezaji thamani madini na maonesho, huku Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akitarajiwa kuufunga Novemba 21, 2026.