Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imesema watumiaji wa bidhaa na huduma za bima nchini wameongezeka kutoka milioni 5.6 mwaka 2021 hadi milioni 26.8 mwaka 2025, mafanikio yanayotokana na usimamizi madhubuti wa sekta hiyo.

Kamishna wa TIRA amesema ongezeko hilo limeifanya sekta ya bima kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa (GDP) kutoka asilimia 1.68 mwaka 2021 hadi asilimia 2.11 mwaka 2025.

Amesema uwiano wa wananchi wanaotumia na kunufaika na huduma za bima umeongezeka kutoka asilimia 8.9 mwaka 2021 hadi asilimia 39.3 mwaka 2025.

Aidha, wastani wa fedha zinazotumiwa na mtu mmoja kwa ajili ya bima umeongezeka kutoka Sh 15,334 mwaka 2021 hadi Sh 37,455 mwaka 2025.

Kamishna huyo amesema ajira rasmi katika sekta ya bima zimeongezeka kutoka 3,737 mwaka 2021 hadi 15,398 mwaka 2025, huku watoa huduma za bima wakiongezeka kutoka 993 hadi 10,940 katika kipindi hicho.

Amesema ada za bima zilizoandikishwa zimeongezeka kutoka Sh bilioni 911 mwaka 2021 hadi Sh trilioni 2.55 mwaka 2025, hatua inayoonesha ukuaji wa shughuli za bima nchini.

Alisema thamani ya madai ya bima yaliyolipwa kwa mwaka imeongezeka kutoka Sh bilioni 397.57 mwaka 2021 hadi Sh trilioni 1.29 mwaka 2025, kuimarisha uwezo wa sekta kuhudumia wateja.

Aidha, thamani ya mali zilizowekezwa na kampuni za bima imeongezeka kutoka Sh bilioni 939.69 mwaka 2021 hadi Sh trilioni 2.24 mwaka 2025.

Amesema mitaji katika soko la bima imeongezeka kutoka Sh bilioni 416 mwaka 2021 hadi Sh trilioni 1.89 mwaka 2025, huku sekta hiyo ikiendelea kuimarisha uwezo wake wa uwekezaji.

Kamishna huyo amesema uwezo wa sekta ya bima kuhimili vihatarishi umefikia Sh trilioni 193.53, sawa na asilimia 94.5 ya Pato la Taifa.

Alisema TIRA imeendelea kuimarisha usimamizi kwa kutumia mifumo ya kidijitali ikiwemo TIRA MIS, ORS, IRIS na TSS Portal, inayorahisisha utoaji wa huduma, leseni, malalamiko na ulipaji wa madai.

Amesema mamlaka hiyo inaendelea kuhakikisha kampuni za bima zinakuwa na mitaji ya kutosha, zinalipa madai kwa wakati, zina mikataba hai ya bima mtawanyo na zinazingatia misingi ya utawala bora.

Aidha, amesema TIRA huchukua hatua stahiki dhidi ya kampuni zinazobainika kuwa katika viashiria vya hatari kubwa, ikiwemo upungufu wa mtaji, malimbikizo ya madai, madeni na kukosa amana ya dhamana Benki Kuu ya Tanzania, ili kulinda wananchi na kuimarisha imani katika sekta ya bima.