Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila akifungua mkutano hu jijini Arusha leo

………..
Na Happy Lazaro, Arusha.
Watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wameendelea kunufaika na huduma za kifedha kupitia PCCB SACCOS, ambayo imetoa mikopo ya Sh bilioni 43.2 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kwa ajili ya kuwawezesha wanachama kuwekeza na kukidhi mahitaji mbalimbali ya maisha.
Mikopo hiyo imetolewa kwa wanachama 5,522 katika kipindi cha Oktoba mwaka jana hadi Septemba mwaka huu, ikihusisha mahitaji ya elimu, ujenzi, biashara, uvuvi na matumizi ya dharura.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 23 wa chama hicho unaofanyika jijini Arusha, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, ameelekeza nguvu katika usimamizi wa fedha za wanachama, akitaka viongozi kuhakikisha kila fedha inatunzwa na kutumika kwa uwajibikaji.
Amesema chama cha ushirika kinapaswa kujengwa katika misingi ya kuaminiana, hivyo amewataka wanachama kutimiza wajibu wao wa kurejesha mikopo kwa wakati ili kuepusha kukwama kwa mzunguko wa fedha na kuwanyima wengine fursa ya kukopa.
Katika hatua nyingine, Chalamila ametoa wito kwa watumishi 400 ambao bado hawajajiunga na PCCB SACCOS kujiunga, akibainisha kuwa ushiriki wao utaongeza wigo wa kunufaika na huduma za chama hicho. Pia amesisitiza elimu ya bima, uwekezaji na matumizi bora ya fedha kuwa muhimu katika kujenga ustawi wa wanachama.
Akitoa taarifa ya mwenendo wa chama, Mwenyekiti wa Bodi ya PCCB SACCOS, Betrod Busanda, amesema matarajio ya chama ni kupata faida ya Sh bilioni 7.3, huku mapato yaliyokusanywa kwa ajili ya bima ya mikopo yakiwa Sh milioni 565 na kinga ya posho Sh milioni 555.
Amefafanua kuwa idadi ya wanachama 5,522 waliotajwa kunufaika na mikopo inajumuisha waliokopa mara kadhaa, wakati wanachama 1,778 ndiyo waliopata mikopo bila kuhesabiwa zaidi ya mara moja.
Naye Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, amewataka wajumbe wa mkutano huo kutumia nafasi ya siku mbili kujadili changamoto na kuweka mikakati itakayochochea maendeleo ya chama, kuboresha huduma zake na kuongeza manufaa kwa watumishi.
