Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yanasaidia kupunguza gharama za matumizi ya nishati majumbani na kuwawezesha wananchi kuokoa fedha kwa ajili ya shughuli nyingine za maendeleo.
Amesema hayo leo, Novemba 15, 2026, alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) kwa wananchi wa Jimbo la Mchinga, mkoani Lindi, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Ameeleza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yana faida nyingi, zikiwemo kulinda mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti inayotumika kuzalisha kuni na mkaa, pamoja na kulinda afya za wananchi dhidi ya madhara yatokanayo na moshi wakati wa kupika.
Amesisitiza kuwa matumizi ya gesi ya kupikia yatasaidia kupunguza athari za kiafya zinazotokana na kuvuta moshi, huku yakiwawezesha wananchi kutumia nishati kwa ufanisi na kupunguza gharama za kupikia.
Aidha, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mhe. Salma Kikwete, kwa jitihada za kuwawezesha wananchi kupata mitungi ya gesi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Ndejembi amewahakikishia wananchi wa Jimbo la Mchinga kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha wanapata huduma ya umeme wa uhakika.
Ameeleza kuwa ifikapo Januari 2027, Jimbo la Mchinga linatarajiwa kupata transfoma mpya yenye uwezo wa KVA 50 kutoka Chalinze, ambayo itafungwa kuchukua nafasi ya transfoma iliyopo ambayo imekuwa ikitumika kwa muda mrefu.
Amesema Serikali imefanya jitihada za makusudi kuhakikisha inapatikana transfoma yenye uwezo unaohitajika ili kuboresha huduma ya umeme na kuwawezesha wananchi kutumia nishati hiyo katika shughuli zao za kijamii na kiuchumi.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara kupitia miradi ya kuunganisha maeneo hayo na Gridi ya Taifa, ikiwemo mradi wa njia ya umeme wa Songea–Tunduru–Masasi.
Ameongeza kuwa hatua inayofuata ni kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa njia ya umeme wa Masasi–Mahumbika inayolenga kuimarisha hali ya umeme katika mikoa husika.

