Kamati ya Ushauri wa Kisheria Mkoa wa Mara imefanya kikao chake cha kwanza kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027, tarehe 13 Novemba 2026, Mkoani Mara.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Wakili wa Serikali Mkoa wa Mara, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Gideon C. Rwechungura ameongoza kikao hicho kilicholenga kuwajengea wajumbe uelewa wa pamoja kuhusu majukumu ya Kamati, kufahamiana na kuweka mikakati ya utekelezaji wa majukumu hayo katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Aidha, Dkt. Rwechungura amesisitiza umuhimu wa Kamati hiyo katika kuimarisha usimamizi na uratibu wa masuala ya kisheria ndani ya Mkoa wa Mara. 

Vilevile, ameeleza umuhimu wa Kamati katika kusaidia kutafuta ufumbuzi wa changamoto na migogoro ya kisheria inayowakabili wananchi.

Katika kikao hicho, Kamati imeweka msingi wa ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja katika kushughulikia masuala ya kisheria yanayohusu Serikali na wananchi. 

Mikakati iliyojadiliwa na Kamati hiyo inalenga kuimarisha ushauri wa kisheria kwa taasisi za Serikali, kulinda maslahi ya umma, na kuhakikisha masuala yote yanayoshughulikiwa yanaongozwa na misingi ya sheria na haki.