Na Hellen Mtereko,

Mwanza

Zikiwa zimesalia siku mbili kuelekea Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), utakaofanyika Jijini Mwanza Novemba 16 hadi 20, 2026 viongozi wa chama hicho wameeleza kuwa mkutano huo ni fursa muhimu ya kuchochea maendeleo na kukuza uchumi.

Mkutano huo umedhaminiwa na Benki ya Azania na unalenga kutoa fursa kwa wananchi, wafanyabiashara na wadau mbalimbali kujifunza, kubadilishana uzoefu, kujenga mitandao ya kibiashara na kutambua fursa mpya zitakazochochea ukuaji wa uchumi.

Hayo yamebainishwa Novemba 12, 2026 na Mwenyekiti wa ALAT Taifa, ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Costantine pamoja na Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa, ambaye pia ni Meya wa Jiji la Mbeya, Dormohamed Issa walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari.

Wamesema mkutano huo si tu jukwaa la kuzikutanisha Serikali za mitaa bali ni kwaajili ya kupata fursa ambazo zinaweza zikatokana na ujio wa Halmashauri 184 ambazo zitashiriki mkutano huo.

“Tunawaomba sana wananchi wa Jiji la Mwanza kujitokeza kwa wingi kwaajili ya kuwakarimu wageni watakaofika kwenye mkutano huo na hii itasaidia kunufaika na fursa mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi”,

Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa na Biashara za Serikali kutoka Benki ya Azania, Samson Mahimbi amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kuwawezesha wananchi na wafanyabiashara kupata maarifa mapya, kutambua fursa za biashara na kuimarisha mahusiano baina ya wadau mbalimbali.

Kwa upande wake Meneja Mahusiano Biashara za Serikali Benki ya Azania, Grace Ngoma, amewaalika wananchi na taasisi za serikali kushiriki katika mkutano huo, ambapo watapata fursa ya kufahamu huduma mbalimbali za kifedha zinazoweza kuwasaidia katika utekelezaji wa miradi yao ya maendeleo.