Jengo la zahanati ya Mnyamasi
Baadhi ya kinamama wakisubiri huduma ya matibabu na watoto wao katika zahanati ya Mnyamasi katika halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi
Baadhi ya kinamama wajawazito wakisubiri huduma katika zahanati hiyo
Baadhi ya kinamama wajawazito wakisubiri huduma katika zahanati hiyo
************************************
Na Mwandishi wetu Katavi
Baadhi ya wakazi wa vijiji vya Mnyamasi, Bariadi, Namhalaja na Msanga katika Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi wameiomba serikali kuongeza idadi ya watumishi wa afya katika zahanati ya Mnyamasi yenye watumishi wanne na inahudumia zaidi ya wananchi 8,000 wa vijiji hivyo hali inayosababisha msongamano mkubwa katika wakati wakisubiri huduma na hivyo kusababisha kero kwa wanawake wajawazito na watoto
Wakizungumza katika zahanati hiyo wananchi hao wamedai kuwa wakati mwingine wanapoteza siku nzima wakisubiri huduma ya matibabu kutokana na kuwepo kwa wingi wa wagonjwa
Benjamin Lucas ni mkazi wa kijiji cha Mnyamasi amesema kutokana na wingi wa wagonjwa watumishi wa zahanati hiyo wanazidiwa na kazi na wakati mwingine wanahudumiwa mpaka nyakati za usiku
“Hasa unapokutwa na malaria hapa utakaa sana mpaka kupata tiba, hali hii inaleta usumbufu mkubwa kwa watoto kwani wanapatwa na njaa”alisema
Ameongeza kuwa endapo serikali itaongeza watumishi basi wataishi kwa raha kwani watakuwa wanapata huduma mapema
Kwa upande wake Bi. Prisca Velianza ambaye ni mkazi wa kijiji cha Bariadi aliyekuwa amemleta mtoto wake kutibiwa amesema alifika zahanati hapo majira ya saa moja na nusu asubuhi na amemaliza kumtibia mwanae saa kumi jioni
Akizungumzia changamoto ya upungufu wa watumishi wa idara ya afya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dk. Omary Sukari amesema wana jumla ya watumishi 836 na wanaohitajika ni watumishi 2120 hivyo kuwa na upungufu wa watumishi 1284
Ameongeza kuwa wanafanya jitihada za kuwaweka watumishi waliopo katika mazingira mazuri ili kuwapa motisha ya kuendelea kufanya kazi kwani wengi wao wapo katika maeneo ya vijijini
Aidha ameeleza kuwa wana mazoea ya kutenga bajeti kwa ajili ya watumishi wapya wanaoajiriwa pale kibali cha kuajiri kinapotoka
Kwa upande wake Sista Elida Machungwa ambaye ni mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto mkoa wa Katavi amekiri kuwepo kwa upungufu wa watumishi hasa wakunga na kusema kuwa wakati mwingine wanalazimika kuhamisha watumishi wenye taaluma hiyo walio wengi katika kituo kimoja kwenda mahali penye changamoto zaidi ili kuwapatia wananchi huduma
Pia ameongeza kuwa wanalazimika kutumia kliniki za mikoba hasa katika maeneo yaliyo mbali na zahanati ili kuwafikia wananchi kwa ajili ya huduma ya mama na mtoto na utoaji wa chanjo mbalimbali