Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt. Fredrick Salukele, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Ndomba akizungumza katika mahafali hayo.jijini Arusha Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Mussa Chacha akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha 

Happy Lazaro, Arusha.

Arusha .SEKTA binafsi na taasisi mbalimbali nchini zimetakiwa kufungua milango ya ajira kwa wahitimu wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), ili kuwawezesha kutumia ujuzi walioupata chuoni katika kujenga maisha yao na kuchangia maendeleo ya taifa.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Mussa Chacha, wakati wa mahafali ya 18 ya ATC yaliyofanyika jijini Arusha, ambapo jumla ya wanafunzi 1,337 wamehitimu katika fani na ngazi mbalimbali za elimu ya ufundi.

Profesa Chacha amesema wahitimu hao wameandaliwa kwa kupata maarifa na ujuzi unaoweza kutumika katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji na huduma, hivyo ni wakati wa waajiri kuwapa nafasi za kuingia katika soko la ajira na kuthibitisha uwezo wao.

Amesema chuo hicho kinatambua umuhimu wa kuandaa wataalamu wanaokidhi mahitaji ya sasa na yajayo ya nchi, hasa katika kipindi ambacho Tanzania inalenga kukuza uchumi kupitia viwanda, teknolojia na matumizi bora ya rasilimali watu.

Akizungumza katika mahafali hayo, Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt. Fredrick Salukele, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Ndomba, amesema elimu ya ufundi ina mchango mkubwa katika kufanikisha maendeleo ya taifa.

Amesema Taifa linahitaji wataalamu ambao hawaishii kuwa na maarifa ya darasani pekee, bali wanaoweza kuyatumia katika kubuni teknolojia, kutengeneza vifaa, kutatua matatizo ya kiufundi na kuboresha mifumo ya uzalishaji.

Amesisitiza kuwa ATC inapaswa kuendelea kuwekeza katika utafiti, ubunifu na mafunzo yanayowapa wanafunzi uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika jamii na sekta mbalimbali za uchumi.

Katika hatua nyingine, Profesa Chacha amesema chuo hicho kimeanzisha utaratibu wa kuwapa nafasi vijana waliopata uzoefu wa ufundi kupitia kufanya kazi kwa vitendo mitaani, ili waweze kupata mafunzo rasmi na kutambua zaidi ujuzi wao.

Amesema mpango huo unatekelezwa kwa kushirikiana na wadau wakiwemo Chama cha Wakandarasi na Watoa Huduma Washirika Tanzania (TUKASA), kwa lengo la kuwaongezea uwezo vijana ambao wamekuwa wakishiriki katika shughuli za ujenzi bila kuwa na mafunzo rasmi.

Amefafanua kuwa, chuo hicho hakitawaacha wahitimu baada ya kumaliza masomo, kwani kitaendelea kuwapatia nafasi za kuimarisha ujuzi wao kupitia programu ya Teaching Factory bila malipo.

Akitoa takwimu za mahafali hayo, amesema wahitimu 444 wamehitimu shahada, 45 shahada za uzamili, 660 stashahada, tisa stashahada za juu, 16 stashahada za awali na 163 mafunzo ya ufundi stadi.

Amesema wahitimu hao wanatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kutumia taaluma zao kuongeza uzalishaji, kuanzisha shughuli za kiuchumi na kuchangia ujenzi wa uchumi wa viwanda na teknolojia.