Na: OWM–TAMISEMI, Nanyumbu – Mtwara
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemthibitishia Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi kuwa ofisi yake itawachukulia hatua za kinidhamu na kisheria viongozi wa ngazi za msingi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa watakaoshindwa kudhibiti uingiaji holela wa mifugo katika maeneo yao ya utawala na kusababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Prof. Shemdoe ametoa ahadi hiyo leo Novemba 12, 2026 akiwa Nanyumbu, alipopewa fursa na Makamu wa Rais Mhe. Ndejembi kueleza kwa wananchi hatua zinazochukuliwa na ofisi yake katika kuzuia migogoro ya wakulima na wafugaji, wakati wa ziara ya kikazi ya Makamu wa Rais yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayowahusu wananchi wa wilaya ya Nanyumbu, mkoani Mtwara.
“Mhe. Makamu wa Rais, kama ulivyotuelekeza, tutawachukulia hatua viongozi wote watakaoshindwa kusimamia sheria na taratibu na kusababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji, kuanzia Mwenyekiti wa Kijiji, Mtendaji wa Kijiji, Mtendaji wa Kata mpaka viongozi wa ngazi za juu,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Akizungumzia uwekezaji katika sekta ya elimu, Prof. Shemdoe amesema ujenzi wa Shule ya Mkoa ya Sayansi ya Wasichana ya Mkapa Girls wenye thamani ya Shilingi Bilioni 4 ni uwekezaji wenye manufaa kitaaluma na kiuchumi kwa wananchi, kwani umeshawishi wananchi wa Mangaka, Nanyumbu, kufungua maduka ya vifaa vya shule yaliyowaongezea kipato. Ameongeza kuwa Serikali imepeleka tena Shilingi Milioni 560 Mangaka kwa ajili ya ujenzi wa shule nyingine ya sekondari.
Ameongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha TARURA inaendelea na ujenzi wa barabara ya lami ya Kambuti yenye urefu wa kilomita moja iliyopo Mangaka, na mwaka wa fedha ujao Serikali italeta Shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya CCM.
Akieleza kuhusu uwekezaji katika afya ya msingi, Prof. Shemdoe amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nanyumbu iliyopo Mangaka na kuongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha ameridhia kiasi cha Shilingi Milioni 500 kutumika kwa ajili ya kuongeza wodi itakayoimarisha huduma za kulaza wagonjwa hospitalini hapo.
Makamu wa Rais Mhe. Deogratius Ndejembi ameanza ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara leo kwa kukagua na kuweka jiwe la msingi mradi wa maji wa Miji 28 katika chanzo cha mto Ruvuma, Mangaka wilaya ya Nanyumbu, ikiwa ni pamoja na kuzungumza na wananchi wa wilaya za Nanyumbu, Masasi, Tandahimba na Newala.
