Na Mwamvua Mwinyi, Kibiti

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Ramadhan Ali Kimara, ameitaka Halmashauri na wadau mbalimbali kutumia uwekezaji wa shamba la mikorosho lenye ukubwa wa ekari 400 katika Kitongoji cha Ugezi, Kata ya Mtawanya, kuwa chachu ya kukuza uchumi wa eneo hilo kupitia uzalishaji wa korosho na ajira kwa vijana.

Alieleza ,uwekezaji huo una manufaa kwa Halmashauri na wananchi kutokana na fursa za ajira zinazopatikana katika shughuli za utunzaji wa shamba na uvunaji wa korosho, huku vijana wakipata nafasi ya kujifunza mbinu bora za kilimo cha kisasa.

Kwa upande wake, msimamizi wa shamba hilo, Gilbert Masawe, alifafanua kuwa shamba hilo lina miaka mitatu tangu kuanzishwa na uzalishaji wake bado haujafikia kiwango cha juu katika eneo lote la ekari 400 kutokana na mikorosho kuendelea kukua.

Alisema matarajio ni kuongeza uzalishaji kadri mikorosho inavyoendelea kukomaa, huku kukiwa na mpango wa kupanua matumizi ya zao hilo kwa kuanza uzalishaji wa mvinyo unaotokana na mabibo ya korosho.

Alieleza kuwa kwa sasa mvinyo huo huzalishwa kwa kiwango kidogo kwa ajili ya matumizi ya wafanyakazi wa shamba hilo, lakini kuna mpango wa kupanua uzalishaji wake siku zijazo ili kuongeza thamani ya zao la korosho na kupanua wigo wa fursa za kiuchumi.