…………………………………………………………………………….
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
BAADHI ya maduka wilayani Kibaha yanauza sukari kwa bei ya sh. 3,200-4,000 kwa kilo ambayo ni kinyume na bei elekezi ya serikali kwa mkoa wa Pwani ambayo ni sh. 2,700.
Kero hiyo imejitokeza kutokana na wauzaji wa maduka ya maeneo mbalimbali ya wilayani ya Kibaha hayana bidhaa hiyo muhimu ,na sasa sukari imekuwa adimu.
Wananchi wakizungumza walisema sukari imekuwa ikiuzwa kwa kificho ambapo wakiwa na wasiwasi wanasema sukari hamna wakiogopa kukamatwa na polisi kutokana na kuuza bei kubwa.
“Baadhi ya maduka wamefunga sukari hiyo kwenye magazeti ikiwa kwenye ujazo wa robo kilo wakikutialia mashaka wanakwambia sukari hakuna wakiwa hawana shaka na wewe wanakuuzia kwa bei kuanzia 3,200 kwa kilo hadi 4,000 kwa maduka ya pembezoni mwa miji,” walisema wananchi hao.
Hata hivyo wananchi hao walishauri hatua pia zichukuliwe kwa wafanyabiashara na mawakala wenye leseni ya kuwauzia wenye maduka kwani wanauza kwa bei kubwa inayosababisha wauzaji wa madukani kuuza bei kubwa kwa wananchi .
Akizungumza suala hilo kamanda wa polisi mkoani Pwani Wankyo Nyigesa aliwataka wananchi waache kulalamika bali watoe taarifa kwa jeshi hilo ili lichukue hatua.
Nyigesa alisema kuwa polisi hawawezi kuangalia wafanyabiashara hao wakivunja sheria kwa kuuza bei ambayo ni kinyume na utaratibu ambao umepitishwa na serikali.
“Tunatoa onyo kwa wafanyabiashara ambao wanakwenda kinyume cha sheria kwa kuuza sukari kwa bei ya juu tofauti na iliyopangwa ili wananchi wasiumie,” alisema Wankyo.
Hadi sasa jeshi la polisi mkoani Pwani linaendelea na msako ,kuwabaini wafanyabiashara ambao wameficha sukari na kuuza kwa bei isiyo elekezi ya sh .2,700 kwa kilo moja ,ambapo ni kinyume cha sheria .
Kutokana na msako huo ulioanza mkoani hapo ,wiki mbili sasa,jeshi hilo ,limeshakamata jumla ya kilo 1,087 za sukari pamoja na watuhumiwa nane wanaodaiwa ni wafanyabiashara walioficha sukari hiyo na mwingine mmoja kati yao kupatikana na sukari isiyolipiwa ushuru.