NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
USHIRIKA wa Umwagiliaji Ruvu (CHAURU) unaofanya kilimo katika mashamba ya Ruvu ,Kata ya Vigwaza Bagamoyo, Pwani, Unahitaji sh .bilioni. 11 kwa ajili ya kununua mashine ya kuondoa maji kwenye mashamba ya wanachama wake.
Hatua hiyo inalenga kuondokana na changamoto ya mashamba kuingia maji, hasa nyakati za mvua hali inayosababisha kushindwa kuendeleza kilimo.
Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa CHAURU Sadala Chacha, alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za mashamba hayo, ambapo alisema suala hilo limepitishwa na wanachama, na tayari wameshapeleka maombi hayo katika benki ya TIB.
“Hatua hii inalenga kuboresha ufanisi kwa wanachama waweze kupata mafanikio zaidi katika sekta ya kilimo ,tumepeleka ombi la pesa kiasi cha sh. bilioni 11 tutazonunua mashine inayonyonya maji yanayotuama mashambani,”; mwaka huu wa kilimo 2019/2020 mashamba yetu yamevamiwa na maji, hivyo kusababisha baadhi yetu kushindwa kupanda,” alisema Chacha.
Aidha Chacha alieleza, CHAURU inakabiliwa na changamoto kubwa ya kutengeneza miundombinu ya mifereji na baadhi ya matuta ya kuzuia maji yasiathiri mashamba.
Nae meneja wa ushirika huo ,Victoria Olotu alieleza pia kuna changamoto ya uwepo wa mnyama Kiboko, anayeonekana kwenye mashamba hayo nyakati za jioni, hali inayosababisha hofu kubwa kwa wana-Ushirika hao.
Alisema kwamba kutokana na hali hiyo ameshatoa taarifa kwa viongozi wanaohusika ili wafike kwa ajili ya kumswaga aweze kuondoka, hatimae wanachama waweze kuendelea na shughuli zao kama kawaida.