Na. OWM – TAMISEMI, Tabora
Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, kupitia Idara ya Usimamizi wa Elimu na Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), chini ya mpango wa Shule Salama awamu ya kwanza, imewakutanisha wadau wa elimu nchini kwa lengo la kuimarisha usalama wa wanafunzi na kuhakikisha wanakamilisha mzunguko wa elimu.
Wadau hao wamekutana mkoani Tabora, ambapo walimu, maafisa maendeleo ya jamii, wenyeviti wa bodi za shule pamoja na wadau wengine wa elimu wamepata fursa ya kujadili na kuwasilishwa kwa mipango, miongozo, kanuni na mbinu mbalimbali za kuhakikisha mazingira ya shule yanakuwa salama na rafiki kwa wanafunzi.
Akizungumzia utekelezaji wa mpango huo, Dkt. Theresia Kuiwite, mratibu wa usalama wa mazingira na jamii katika mradi huo, amesema mpango huo unaangazia maeneo mbalimbali, ikiwemo upatikanaji wa chakula shuleni, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi, kuimarisha huduma za ushauri nasaha na malezi, pamoja na kukabiliana na matumizi ya adhabu ya viboko shuleni.
Amesema hatua hizo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazoweza kuhatarisha usalama wa wanafunzi na kusababisha baadhi yao kukatisha masomo.
Mpango huo unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo, umefanikiwa kufikia shule 3,392, lengo la awali la kufikia shule 2,000, kwa kuimarisha mifumo ya kukabiliana na changamoto zinazohatarisha usalama na ustawi wa wanafunzi.
Kupitia ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wa elimu, mpango huo unalenga kujenga mazingira yatakayomwezesha kila mwanafunzi kupata elimu katika mazingira salama, yenye haki na yanayompa nafasi ya kukamilisha masomo yake.

