
Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Kinondoni Elizabeth Mokiwa akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 11, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026.
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Kinondoni, imefuatilia matumizi ya fedha katika miradi 14 ya maendeleo yenye thamani ya Sh bilioni 81.2, ikiwemo ujenzi wa viwanja vitatu vya mazoezi vya Leaders Club, Gymkhana na Farasi, vitakavyotumika katika mashindano ya AFCON 2027.
Miradi hiyo ina thamani ya jumla ya Sh 81,222,258,864.01, huku mradi wa ujenzi wa viwanja hivyo vitatu ukigharimu Sh 51,595,248,113.20.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 11, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Elizabeth Mokiwa, amesema ufuatiliaji huo umebaini mapungufu mbalimbali katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Mokiwa amesema baada ya kubaini changamoto hizo, TAKUKURU ilifanya vikao kazi na wadau wa utekelezaji wa miradi, wakiwemo wakandarasi, washauri na wasimamizi, pamoja na Ofisi ya Mdhibiti Ubora, kwa lengo la kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati na kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Amesema baadhi ya mapungufu yaliyobainika tayari yamefanyiwa kazi, huku mengine yakiendelea kushughulikiwa.
Katika hatua nyingine, amesema taasisi hiyo imefanikisha ukusanyaji wa Sh 37,120,799 kama ushuru na adhabu kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya kubaini uingizaji wa madumu 510 ya mafuta ya kula, yenye ujazo wa lita 20 kila moja, kwa njia za magendo kupitia Pwani ya Kunduchi.
Amesema TAKUKURU ilifanya ufuatiliaji katika eneo hilo na kukamata gari lililokuwa limebeba shehena hiyo, ambapo uchunguzi ulibaini kuwa mwagizaji hakuwa na nyaraka halali za kuingiza bidhaa nchini wala uthibitisho wa kulipa kodi na ushuru stahiki.
Ameongeza kuwa kwa kushirikiana na TRA, hatua za kisheria zilichukuliwa dhidi ya mwagizaji na mmiliki wa gari, huku kiasi hicho cha fedha kikilipwa kama ushuru na adhabu.
Amesema TAKUKURU itaendelea kushirikiana na TRA pamoja na taasisi nyingine za Serikali katika kudhibiti ukwepaji kodi na uingizaji wa bidhaa kwa njia za magendo ili kulinda uchumi wa Taifa.
Kuhusu utoaji wa elimu, Mokiwa amesema TAKUKURU Kinondoni kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu madhara ya rushwa na umuhimu wa kushiriki katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo.
Aidha, amesema katika kipindi hicho jumla ya malalamiko 110 yalipokelewa, ambapo 47 yalihusu rushwa na 63 hayakuhusiana na rushwa. Uchunguzi wa malalamiko yote 47 yanayohusu rushwa unaendelea katika hatua mbalimbali, huku waliowasilisha malalamiko yasiyohusu rushwa wakipewa ushauri stahiki.
Katika upande wa mashauri ya mahakamani, amesema kesi 14 zinaendelea, huku kesi mpya 10 zikifunguliwa katika kipindi hicho. Pia, kesi 12 zilitolewa maamuzi, ambapo Jamhuri ilishinda kesi tisa.
Akizungumzia mikakati ya taasisi hiyo, Mokiwa amesema itaendelea kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali katika miradi ya maendeleo, kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu kuzuia rushwa, pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya Programu ya TAKUKURU Rafiki.
Amewataka wananchi kujiepusha na vitendo vya rushwa na kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo kwa kutoa taarifa wanapobaini viashiria vya rushwa kupitia namba 113, bila malipo.
“Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu; Tutimize Wajibu Wetu.”
