Serikali imeondosha sintofahamu kati ya wakulima na wafugaji katika eneo la Sanga Sanga, Morogoro kwa kujenga birika la kunyweshea mifugo na miundombinu ya majisafi na salama kwa matumizi ya nyumbani.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Patrick Mwalunenge (Mb), ameiongoza kamati kukagua mradi huo unaohudumia zaidi ya mifugo elfu mbili kwa siku, pamoja na matumizi ya nyumbani kwa wakazi wapatao 1,400.
Amepongeza ubunifu uliotumika na Wizara ya Maji ambapo kiasi cha lita za ujazo elfu 15,562 zinazalishwa kwa saa katika kisima chenye urefu wa mita 110.
Uwepo wa mradi huo wa kisima ni sehemu ya uhifadhi wa bwawa la Mindu, ambapo utamaduni wa kuswaga mifugo kuipeleka mtoni kunywa maji umekoma, pia kuharibu mashamba ya wakulima.
Mhe. Mwalunenge ameainisha kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo, asasi ya kimataifa ya masuala ya maji iitwayo World Waternet imesaidia kufanikisha kazi hiyo.
Amewataka wananchi kuendelea na utamaduni wa kupenda mazingira na kuotesha miti ili kuwa na uhakika wa huduma endelevu ya maji.
Katika hatua nyingine, ametaka kazi ya udabuaji wa mto Ngerengere eneo la Kihonda ikamilike mapema na matete pamoja na miti ioteshwe kwa kushirikiana na wananchi ambapo Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu itafanya kazi ya kuanisha miti rafiki wa maji.
Amesema kazi hiyo inalinda maslahi ya wananchi na mali zao.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri , kwa niaba ya Waziri wa Maji ameahidi kufanyia kazi maelekezo yote ya kamati. Pia ameishukuru asasi ya World Waternet kwa kushirikiana na serikali katika huduma ya maji na uhifadhi wa mazingira, na kuahidi ushirikiano huo kuimarishwa zaidi.

