Wajasiriamali wa Manispaa ya Kibaha walionufaika na mikopo ya asilimia 10 isiyokuwa na riba wametakiwa kuwa waaminifu na kurejesha fedha hizo kwa wakati ili kutoa fursa kwa vikundi vingine vinavyohitaji mikopo hiyo kuweza kunufaika.
Wito huo umetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, alipokutana na vikundi mbalimbali vya wajasiriamali kutoka Kata ya Tangini vilivyonufaika na mikopo hiyo.
Dkt. Nicas amesema amefurahishwa na vikundi alivyokutana navyo, ambavyo vilifanikiwa kupata mikopo katika awamu iliyopita na kurejesha kwa wakati, huku baadhi yake vikiomba tena mikopo katika dirisha hili, akieleza kuwa anaamini vitaendelea kuwa waaminifu katika urejeshaji.
Amesema baadhi ya vikundi kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati kunasababisha vikundi vingine kukosa fursa ya kupata fedha hizo, ambazo zimetolewa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuwawezesha wanawake, vijana na makundi maalumu kuinua hali zao za kiuchumi.
Aidha, amevitaka vikundi hivyo kujisajili BRELA na kuwa kampuni, kisha kujisajili katika mfumo wa NEST ili viweze kunufaika na fursa za zabuni zinazotangazwa na Halmashauri, akieleza kuwa sheria inaelekeza asilimia 30 ya zabuni kutolewa kwa wazawa, hususan vikundi vilivyonufaika na mikopo ya asilimia 10.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo wa Manispaa ya Kibaha, Mkaminoela Hangaya, amesema katika dirisha hili vikundi 120 vimepitishwa kwa ajili ya kupatiwa mikopo hiyo isiyokuwa na riba na kwamba muda si mrefu vitapatiwa fedha hizo.
Amesema katika mchakato huo wamezingatia makundi yote, yakiwemo ya watu wenye ulemavu, wanawake na vijana, ambao watapatiwa mikopo kupitia dirisha la Septemba, huku akiwataka watakapopokea fedha hizo kuhakikisha wanazirejesha kwa wakati.
Naye Afisa Maendeleo wa Kata ya Tangini, Mwanawetu Mohamed, amemshukuru Mstahiki Meya kwa kukutana na wajasiriamali hao, akieleza kuwa baadhi ya vikundi vilivyokutana naye vilinufaika na mikopo katika awamu ya kwanza, vikairejesha kwa wakati na sasa vimeomba tena katika dirisha jipya.
Mstahiki Meya ameendelea kukutana na makundi mbalimbali ya wananchi, akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kuona wananchi wanapata fursa za kujiinua kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 isiyokuwa na riba kwa wanawake, vijana na makundi maalumu.

