Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Usultani wa Oman zimesaini Mkataba na Hati ya Makubaliano ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za uchukuzi wa majini na mafunzo ya kidiplomasia. Nyaraka hizo zimesainiwa Novemba 10, 2026, visiwani Zanzibar, wakati wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya nchi hizo, ngazi ya Mawaziri.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Mhe. Sayyid Badr bin Hamad bin Hamood Albusaidi.

Mkataba wa sekta ya uchukuzi unahusu utambuzi wa pamoja wa vyeti vya umahiri na ustadi wa mabaharia, kwa kuzingatia viwango vya Mkataba wa Kimataifa wa STCW wa mwaka 1978. Hatua hiyo itarahisisha utambuzi wa vyeti vya mabaharia wa nchi hizo na kuongeza fursa za ajira katika meli za Tanzania na Oman.

Hati ya pili inalenga kuimarisha ushirikiano katika mafunzo na elimu ya kidiplomasia kati ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na Chuo cha Diplomasia cha Oman, kupitia kubadilishana wataalamu, wakufunzi na wanafunzi, pamoja na kuandaa mafunzo, semina na tafiti za pamoja.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Waziri Kombo amesema kuwa Mkataba na Hati ya Makubaliano hiyo vitaongeza wigo wa fursa za ushirikiano katika sekta husika, huku vikichangia kuimarisha uwezo wa kitaalamu na kuongeza manufaa kwa wananchi wa nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Waziri Albusaidi amesisitiza dhamira ya Oman ya kuendeleza na kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kirafiki na Tanzania, kupitia ushirikiano wa karibu katika maeneo mbalimbali yenye maslahi ya pamoja.

Aidha, viongozi hao wameeleza kuwa ushirikiano huo una nafasi kubwa ya kukuza ushirikiano katika nyanja za kiuchumi, kidiplomasia na kijamii, pamoja na kufungua fursa mpya za maendeleo kwa wananchi wa nchi hizo mbili.