Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka viongozi wanaosimamia miradi ya maendeleo kuacha kubembelezana na wakandarasi wanaoshindwa kutimiza wajibu wao, akionesha kukerwa na ucheleweshaji wa ujenzi wa Soko la Manzese A na B, mjini Songea.

Mradi huo, ambao mkataba wake ulianza mwaka 2025 kwa kipindi cha miezi 18 na ulitarajiwa kukamilika Septemba 2026, umechelewa licha ya mkandarasi kulipwa shilingi bilioni 3 kama malipo ya awali.

Akizungumza na wananchi wa Songea, wakati wa ziara yake mkoani Ruvuma, Makamu wa Rais amembana kwa maswali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Wakili Bashir Muhoja, akitaka kufahamu sababu za mkandarasi huyo kuongezewa muda wa utekelezaji hadi Machi 2027, wakati tayari imebainika kuwa anakabiliwa na udhaifu wa usimamizi na upungufu wa vifaa vya kazi.

“Hebu tubadilike! Tuwe accountable na fedha za umma. High-level meeting inakusaidia nini?” amehoji Ndejembi, akipinga utaratibu wa viongozi kuendelea kufanya vikao vya kumbembeleza mkandarasi badala ya kuchukua hatua zinazohakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Makamu wa Rais amemtaka Waziri mwenye dhamana ya TAMISEMI kuchukua hatua dhidi ya uzembe katika usimamizi wa mradi huo, akisisitiza kuwa viongozi lazima wawajibike kwa dhamana walizopewa.

Aidha, ameiagiza TAKUKURU kuchunguza kampuni iliyopewa mradi huo, ikiwemo matumizi ya fedha za malipo ya awali, ili kubaini sababu za mkandarasi kushindwa kutekeleza wajibu wake licha ya kupokea fedha za walipakodi.

Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Serikali haiwezi kuvumilia uzembe unaosababisha wananchi kuendelea kupata kero, huku fedha nyingi za umma zikiwa zimetumika bila miradi kukamilika kwa wakati.

Kauli ya Makamu wa Rais imebeba ujumbe mzito kwa viongozi na watendaji wa Serikali: Fedha za wananchi si za kubembelezana na wakandarasi; kila mwenye dhamana ya kusimamia miradi ya maendeleo lazima awajibike.

Makamu wa Rais anaendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa wa Ruvuma, akitarajiwa kuelekea mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.