MTWARA: Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imewahakikishia wawekezaji wa viwanda vya kubangua korosho nchini upatikanaji wa malighafi za kutosha, ikisisitiza kuwa haitakubali viwanda vilivyojengwa kwa gharama kubwa kushindwa kufanya kazi kutokana na uhaba wa korosho ghafi.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Francis Alfred, ametoa kauli hiyo Novemba 7, 2026, katika kikao cha wadau wa korosho kilichoandaliwa na Benki ya NMB mkoani Mtwara. Amepongeza ushirikiano wa benki hiyo na wafanyabiashara, huku akizihimiza taasisi nyingine za fedha kuunga mkono sekta hiyo na kuhakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Biashara ya Kilimo kwa Wateja Wakubwa wa NMB, Christopher Mwalugenge, amesema benki hiyo imejipanga kutoa masuluhisho ya kifedha kwa wanunuzi wa minada, masoko ya awali, wabanguaji na wasafirishaji wa korosho nje ya nchi katika msimu wa 2026/2027.
Amesema huduma hizo zinalenga kurahisisha upatikanaji wa mitaji, ununuzi wa korosho kwa wakati, utekelezaji wa mikataba ya kimataifa na malipo katika mnyororo wa thamani wa zao hilo, hatua inayotarajiwa kuchochea biashara na kusaidia juhudi za kuongeza uwezo wa viwanda vya kubangua korosho nchini ifikapo mwaka 2030.