Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Darsh Industries Limited ,Bhadresh Pandit akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026, linalofanyika katika viwanja vya TGT jijini Arusha.
Mkurugenzi wa masoko wa kampuni hiyo, Darsh Pandit akizungumza na waandishi wa habari jijiji Arusha
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha .WAKULIMA wametakiwa kuongeza uzalishaji kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya viwanda na masoko nje ya nchi kwani kuna fursa kubwa ya masoko kutokana na ongezeko la mahitaji kwa ajili ya usindikaji wa vyakula na upanuzi wa masoko ya ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa jijini Arusha leo na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Darsh Industries Limited inayozalisha bidhaa za vyakula kupitia chapa ya Red Gold ,Bhadresh Pandit wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026, linalofanyika katika viwanja vya TGT jijini Arusha.
 Bhadresh amesema kampuni hiyo ina viwanda viwili vilivyopo Arusha na Iringa, vinavyoshirikiana kwa karibu na wakulima ili kupata mazao yanayotumika kuzalisha bidhaa mbalimbali za chakula.
Ameongeza kuwa ,kampuni hiyo inahitaji mazao yakiwemo nyanya, pilipili mbuzi, pilipili mwendokasi, karanga na matunda mbalimbali kama machungwa, mananasi na matunda damu, ambayo hutumika kama malighafi katika uzalishaji.
Ameeleza kuwa kupitia mazao hayo kampuni huzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo michuzi (sauces), jam na bidhaa nyingine za vyakula, huku ikiendelea kuimarisha uzalishaji wa bidhaa zilizoandaliwa kwa matumizi ya moja kwa moja (Ready to Eat).
“Moja ya malengo ya kushiriki maonesho hayo ni kutangaza bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo, pamoja na kukutana na wakulima ili kujenga ushirikiano utakaowawezesha kulima mazao yenye soko la uhakika.”amesema Bhadresh.
Amesisitiza kuwa kilimo kina fursa kubwa ya kibiashara, hivyo wakulima wanapaswa kuongeza uzalishaji ili kunufaika na mahitaji ya viwanda vinavyotegemea mazao ya ndani.
Akizungumzia fursa za soko, amesema michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani inatarajiwa kuongeza idadi ya wageni watakaotembelea nchi na kutumia huduma mbalimbali ikiwemo hoteli, ambazo ni miongoni mwa maeneo yanayopatikana bidhaa za kampuni hiyo.
Ameongeza kuwa, ongezeko la wageni na matumizi ya bidhaa hizo linaweza kuongeza mauzo ya kampuni, kupanua uzalishaji na kutoa nafasi ya kuongeza ajira kwa Watanzania.
“Ukuaji wa biashara hiyo utaongeza pia manunuzi ya mazao kutoka kwa wakulima wa ndani na kuchangia mapato ya serikali kupitia ulipaji wa kodi.”amesema Bhadresh.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kutumia bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo kwa wingi ili kusaidia kukuza viwanda vya ndani, kuongeza ajira na kupanua soko la mazao yanayozalishwa na wakulima.
Aidha ameiomba serikali kuendelea kuwawezesha wakulima na kutatua changamoto zinazowakabili ili waweze kuzalisha mazao kwa wingi na ubora unaohitajika na viwanda.
Amesema kampuni hiyo tayari inauza bidhaa zake katika nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Malawi na Zambia, huku ikilenga kupanua zaidi masoko yake.
Amesisitiza kuwa ili kufikia malengo hayo, ni muhimu kuimarisha ushirikiano kati ya wakulima, viwanda na serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za kutosha, kukuza uzalishaji wa ndani na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Amefafanua kuwa ,kiwanda hicho cha kusindika nyanya kilichopo mkoani Iringa kina uwezo wa kuchakata zaidi ya tani 250 za nyanya kwa siku, huku kikiendelea kupokea mazao kutoka kwa wakulima wanaotaka kuingia katika ushirikiano wa kibiashara na kampuni hiyo.
Mkurugenzi wa masoko wa kampuni hiyo, Darsh Pandit amewahamasisha vijana nchini kuwekeza katika kilimo kwa kuwa ni sekta yenye fursa kubwa za kiuchumi, huku ikiwataka wakulima kutumia fursa ya kuuza mazao yao moja kwa moja viwandani.
Pandit, amesema kampuni hiyo inajihusisha na usindikaji wa mboga na matunda kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbalimbali za chakula.
“Kampuni hii inazalisha bidhaa zaidi ya 40, zikiwemo tomato paste, tomato sauce, pilipili na siagi ya karanga (peanut butter), huku bidhaa zake zikitambulika kupitia chapa ya Red Gold ambayo imepata hadhi ya Superbrand katika Afrika Mashariki.”amesema Pandit.
Amesema kampuni hiyo imewekeza katika viwango vya ubora kwa kupata vyeti vya TBS, ISO na Halal, hatua inayolenga kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa katika masoko ndani na nje ya nchi.
“Kampuni yetu inashirikiana na wakulima zaidi ya 5,000 kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Iringa, Morogoro na Arusha, ambapo hununua mazao moja kwa moja kutoka kwa wakulima ili kuhakikisha upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya uzalishaji.”amesema .
Amefafanua kuwa, kiwanda chao cha kusindika nyanya kilichopo mkoani Iringa kina uwezo wa kuchakata zaidi ya tani 250 za nyanya kwa siku, huku kikiendelea kupokea mazao kutoka kwa wakulima wanaotaka kuingia katika ushirikiano wa kibiashara na kampuni hiyo.
Ameongeza kuwa kiwanda kikuu cha kampuni hiyo, kipo eneo la Njiro jijini Arusha na kuwataka wakulima wenye mazao yanayohitajika kufika viwandani hapo ili kupata maelekezo kuhusu namna ya kuanzisha ushirikiano wa kibiashara.
