KIPIMO CHETU CHA KUTOA HUDUMA KIWE
📌 Huduma bora kwa wateja ikiwemo lugha ya staha kwa wagonjwa na wepesi wa huduma
📌Kuzuia maambukizi
📌Kupunguza vifo
📌Uchukuaji na utunzaji wa Taarifa za mgonjwa
📌Usafi
Na: David Kavindi, PICHA: Jeremiah Mbwambo
Novemba 09, 2026 – DODOMA
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Prof. Abel Makubi, amewataka wauguzi kuendana na mabadiliko ya mahitaji ya wagonjwa kwa kutumia mbinu bunifu za utoaji wa huduma, kuimarisha mawasiliano na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuongeza ubora wa huduma na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.
Ameyasema hayo leo, Novemba 9, 2026, katika kikao na wauguzi wa hospitali hiyo, ambapo amesisitiza kuwa mabadiliko ya maisha yanahitaji watumishi wa afya kubadili namna wanavyowahudumia wagonjwa kwa kuzingatia utu, unyenyekevu na matumizi ya lugha nzuri wanapokuwa wodini.
Akizungumzia umuhimu wa kuendana na wakati, Prof. Makubi ameeleza kuwa mahitaji ya wagonjwa wa kizazi cha sasa ni makubwa zaidi, hivyo wauguzi wanapaswa kuwa wabunifu badala ya kutegemea mbinu za zamani katika utoaji wa huduma.
“Maisha yamebadilika na mahitaji ya wagonjwa wa sasa ni tofauti. Hatuwezi kuendelea kutumia njia zilezile za zamani katika kuwahudumia wagonjwa. Tunahitaji kuwa wabunifu, kwenda na wakati na zaidi kuwa na unyenyekevu mkubwa katika kuwahudumia.” Amesema prof Makubi
Kwa upande mwingine prof Makubi , amesisitiza umuhimu wa kuzingatia usafi katika wodi na maeneo yote ya kuwahudumia wagonjwa, akieleza kuwa mazingira safi ni sehemu muhimu ya kulinda usalama wa wagonjwa na kuzuia maambukizi yanayoweza kujitokeza wakati wa matibabu.
Hospitali ya Benjamin Mkapa inaendelea kuimarisha huduma zinazomweka mgonjwa katika nafasi ya kwanza kwa kuzingatia usalama, utu, heshima, usafi wa mazingira na ubora wa huduma katika kila hatua ya matibabu.

