Na Happy Lazaro,Arusha .
MakamuĀ wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amefungua rasmi maonyesho ya kimataifa ya mbogamboga, matunda na maua ya HortiLogistica Africa 2026, leo tarehe 09 Novemba 2026 katika Viwanja vya TGT jijini Arusha.
Maonyesho hayo ya siku 3 yanalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji wa mazao ya bustani barani Afrika, yakiwakutanisha zaidi ya washiriki 3,000 kutoka nchi 42 duniani.
Ndejembi ameielekeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TAN TRADE) kuongeza juhudi za kutafuta na kupanua masoko ya kimataifa kwa kubaini kwa usahihi bidhaa zinazohitajika na viwango vya ubora vinavyotakiwa.
“Hatua hii itawasaidia wazalishaji nchini kuendana na mahitaji ya wanunuzi wa kimataifa, kuongeza ushindani wa bidhaa zao na kupanua mauzo nje ya nchi,” amesisitiza Ndejembi.
Aidha, Ndejembi ametoa maelekezo kwa Wizara ya Kilimo kuongeza jitihada katika kuendeleza kilimo cha parachichi ili kukuza mapato ya fedha za kigeni.
Aidha amesema maeneo makuu yanayotakiwa kupewa msukumo wa haraka ni pamoja na Kuimarisha mifumo ya uhifadhi wa mazao,
Kuongeza uzalishaji wa miche bora ya matunda na mbogamboga,Kutoa mafunzo kwa vijana ili kuwavutia kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa kilimo cha mbogamboga.
Aidha Ndejembi amepongeza mchango wa sekta binafsi kupitia Chama cha Wakulima wa Mazao ya Bustani Tanzania (TAHA) kwa kuwezesha wakulima na wajasiriamali wadogo kushiriki katika uzalishaji na biashara ya mazao ya bustani.
Washiriki hao ni pamoja na wakulima, wanunuzi wa kimataifa, wasafirishaji, wawekezaji, pamoja na kampuni za teknolojia.
Maonyesho haya yameandaliwa na TAHA kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Katika maonyesho hayo, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) nayo inashiriki kwa kuonyesha tafiti na teknolojia mpya za kilimo cha bustani, fursa za uhaulishaji wa teknolojia, na kujenga ushirikiano wa kimkakati na wadau wa sekta hiyo.

