BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imefuta leseni ya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni ya kampuni ya Farizal Forex Bureau Limited baada ya kubaini ukiukwaji wa sheria, kanuni na masharti yaliyowekwa katika utoaji wa leseni hiyo.
Hatua hiyo imetangazwa Novemba 9, 2026, kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel M. Tutuba, ikieleza kuwa uamuzi wa kufuta leseni hiyo umeanza kutekelezwa tangu Oktoba 5, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, BoT imechukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa kampuni hiyo imeshindwa kuzingatia vigezo na masharti ya leseni yake, pamoja na kukiuka matakwa ya Sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 na kanuni zilizowekwa chini ya sheria hiyo.
Kutokana na uamuzi huo, Farizal Forex Bureau Limited hairuhusiwi tena kuendesha shughuli za biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa kutumia leseni iliyofutwa.
Hatua hiyo ni sehemu ya usimamizi wa Benki Kuu katika kuhakikisha kuwa watoa huduma za kubadilisha fedha za kigeni wanaendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na masharti ya leseni, ili kulinda uadilifu wa sekta ya fedha nchini.
BoT imeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kutumia huduma za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni yaliyoidhinishwa kisheria na kuzingatia matakwa ya mamlaka husika katika kufanya miamala ya fedha za kigeni.
