Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, amesisitiza umuhimu wa Tanzania na Oman kuweka mikakati madhubuti, kuondoa vikwazo vilivyopo na kubainisha muda maalumu wa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa, ili kuimarisha zaidi ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili.

Balozi Dkt. Shelukindo ameyasema hayo Novemba 9, 2026, visiwani Zanzibar, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Makatibu Wakuu na Wataalam kutoka Tanzania na Oman, unaolenga kutathmini maeneo ya ushirikiano kuelekea Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC).

Amesema kuwa, ili ushirikiano huo uweze kuleta matokeo yanayotarajiwa, ni muhimu kuwepo kwa dhamira thabiti, mikakati inayotekelezeka na ufuatiliaji wa karibu wa makubaliano, hususan katika sekta za biashara, uchukuzi, uwekezaji na kilimo. Aidha, ameeleza kuwa uhusiano wa kihistoria na kindugu uliopo kati ya Tanzania na Oman ni msingi muhimu wa kujenga ushirikiano wa kimkakati utakaowanufaisha wananchi wa nchi zote mbili.

Katika mkutano huo, wajumbe wamepitia na kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa katika Mkutano wa Pili wa JPC uliofanyika jijini Muscat, Oman, mwaka 2022. Vilevile, wamejadili vipaumbele vipya vya ushirikiano vinavyoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, vikiwemo biashara na uwekezaji, uchukuzi, mifugo na uvuvi, nishati na madini, elimu, uchumi wa buluu na kilimo.

Mkutano huo unaoongozwa na kaulimbiu isemayo, “Kutoka Urafiki wa Kihistoria Hadi Ushirikiano wa Kimkakati: Kuendeleza Biashara, Uwekezaji na Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi,” unatarajiwa kuhitimishwa Novemba 10, 2026, kwa mkutano wa ngazi ya Mawaziri. 

Katika mkutano huo, Tanzania na Oman zinatarajiwa kusaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta mbalimbali za kimkakati, hatua inayotarajiwa kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kupanua fursa za maendeleo kwa mataifa hayo mawili.