Na OWM (KAM) – Kigali
Tanzania imeibuka mshindi na kupata tuzo nne kati ya sita katika Maonesho ya 26 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki, maarufu kama Jua Kali – Nguvu Kazi, yaliyofanyika katika Viwanja vya Gikondo, Kigali, Rwanda.
Katika maonesho hayo yaliyofungwa leo,(Novemba 08,2026) wajasiriamali wa Tanzania waliibuka washindi katika makundi mbalimbali. Anne Crochet aliibuka mshindi wa kwanza katika kundi la bidhaa za nguo za batiki, Sima Candle akashinda kundi la ubunifu, sanaa, fenicha na madini, huku Pishon Honey na Makai Moringa wakishika nafasi ya pili na tatu katika kundi la mbogamboga. Tuzo ya nne imechukuliwa na Afritech katika kundi la bidhaa za ngozi.
Kufuatia ushindi huo, Tanzania imekuwa mshindi wa pili kwa ujumla kupitia mjasiriamali Anne Crochet, huku Kenya ikishika nafasi ya kwanza kupitia Thonge Leather na nafasi ya tatu pia ikienda Kenya kupitia Mamlo Foods.
Akizungumza katika ufungaji wa maonesho hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda, Juan Haguma, amesema Serikali ya Rwanda imefarijika kuona wajasiriamali zaidi ya 2,000 wakishiriki kuonyesha na kufanya biashara, hatua inayokuza uchumi na kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Bw. Haguma amewasihi wajasiriamali kuendeleza ubunifu na kutumia teknolojia rahisi ili kuongeza thamani ya bidhaa, hatua itakayosaidia kuongeza uhakika wa masoko ndani ya Afrika Mashariki na nje ya Bara la Afrika.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki, Josephat Rweyemamu, amesema anashukuru kuwa maonesho ya mwaka huu yamewezesha washiriki kupata masoko mapya ya bidhaa zao pamoja na kukuza ushirikiano baina ya nchi wanachama.
Rweyemamu ameongeza kuwa mafanikio ya maonesho hayo yamechangiwa na Serikali ya Rwanda kuimarisha amani na usalama muda wote, hatua iliyosaidia wajasiriamali kufanya biashara zao vizuri bila vizuizi.
Mwenyekiti huyo amewataka wajasiriamali kutoka nchi zote nane kujiandaa kwa maonesho ya mwaka ujao 2027 kwa kuzalisha bidhaa bora na zilizoongezwa thamani, hatua itakayokuza masoko.
Mwakilishi wa AfCFTA, Madame Nomalanga Pearl Gule, amesema wajasiriamali ni mhimili wa uchumi katika Bara la Afrika, ambapo mchango wa wanawake na vijana unaendelea kuhitaji mitaji na mazingira wezeshi, ikiwemo teknolojia.
Ameongeza kuwa AfCFTA inahitaji kuona wajasiriamali wakiwa washiriki katika ukuzaji wa biashara, ambapo itaendelea kushawishi mataifa kuondoa vikwazo kwa wajasiriamali, ikiwemo mipakani, gharama za usafirishaji na taratibu za forodha.
Katika hatua nyingine, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umetunukiwa cheti cha mshiriki bora wa utoaji elimu ya hifadhi ya jamii kwa wajasiriamali, hatua inayolenga kuwajengea uwezo wa kumudu na kuwa na uhakika wa mafao ya uzeeni, ikiwemo tiba.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Tanzania wakati wa ufungaji wa maonesho hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Alana Nchimbi, ameishukuru Serikali ya Rwanda kwa mapokezi na ushirikiano uliofanikisha maonesho hayo, ikiwemo mazingira mazuri na usalama muda wote Watanzania walipokuwa Jijini Kigali.
Maonesho hayo yalifanyika kuanzia Oktoba 30 hadi Novemba 8, 2026, ambapo Tanzania iliwakilishwa na washiriki zaidi ya 374.

