Waandishi wa Habari nchini wametakiwa kuhakikisha uhuru wa habari hautumiki kama mwanya wa kusambaza taarifa zisizothibitishwa, kukashifu au kuvunja utu wa watu, hususan katika kipindi hiki ambacho matumizi ya teknolojia ya Akili Unde (AI) yanaongeza kasi ya uzalishaji na usambazaji wa maudhui.

Wito huo umetolewa leo tarehe 9 Novemba, 2026, na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari wa Azam Media katika siku ya kwanza ya mafunzo ya siku tatu kwa chombo hicho yaliyofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Bodi, jijini Dar es Salaam.

Wakili Kipangula amesema uhuru wa habari una thamani unaposaidia jamii kupata ukweli, kufanya maamuzi sahihi na kuwawajibisha wenye mamlaka bila kukiuka sheria, maadili na haki za watu wengine.

“Uhuru wa habari si uwezo wa kusema kila kitu, bali ni hekima ya kutafuta ukweli, ujasiri wa kuusema na dhamira ya kuwajibika kwa kile kinachosemwa. Sheria huulinda uhuru, maadili huupa mwelekeo na weledi huupa thamani,” amesema Wakili Kipangula.

Amesema kasi ya maendeleo ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya AI, imeongeza wajibu wa Mwandishi wa Habari kuhakiki taarifa, picha, sauti na video kabla ya kuzitumia au kuzisambaza kwa umma.

Kwa mujibu wa Wakili Kipangula, kutanguliza kasi ya kuchapisha habari bila kujiridhisha na ukweli wake kunaweza kuharibu sifa za watu, kupotosha jamii na kupunguza imani ya wananchi kwa Waandishi na vyombo vya habari.

“Ni lazima tuhakikishe taarifa tunazochapisha hazivunji utu wa mtu, hazimkashifu wala kumpotosha mwananchi. Ongezeko la matumizi ya AI linatulazimisha kuwa makini zaidi katika kuhakiki kila taarifa tunayopokea kabla ya kuisambaza,” amesisitiza.

Aidha, amewataka Waandishi wa Habari kuifahamu na kuzingatia Sheria ya Huduma za Habari pamoja na sheria nyingine zinazogusa utekelezaji wa majukumu yao, ikiwemo Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Kwa upande wake, Dkt. Egbert Mkoko, akiwasilisha mada kuhusu maadili katika uandishi wa habari, amesema maamuzi ya kitaaluma yanapaswa kuzingatia maadili yanayokubalika katika jamii bila kwenda kinyume na sheria za nchi.

Ameeleza kuwa jambo linaweza kuonekana kuwa la kawaida au kukubalika katika jamii, lakini likawa na athari za kisheria, hivyo Waandishi wa Habari wanapaswa kupima kwa makini maslahi ya umma, haki za wahusika na madhara yanayoweza kusababishwa na taarifa kabla ya kuichapisha.

“Tunawasisitiza Waandishi wa Habari kuandika habari zinazozingatia maadili ya kitaaluma, lakini maadili hayo pia yaendane na sheria za nchi,” amesema Dkt. Mkoko.

Mafunzo hayo yanayowashirikisha Waandishi wa Habari, waandaaji wa vipindi, Watangazaji wa Redio na Televisheni, Wapiga picha na Wahariri zaidi ya 90 ni sehemu ya jitihada za JAB za kuimarisha weledi, uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria na maadili miongoni mwa Waandishi wa Habari nchini, ili kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi, salama na zenye manufaa