Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
SERIKALI imetoa wito kwa vyuo vikuu, taasisi za utafiti na sekta binafsi kuhakikisha tafiti zinazohusu tiba asilia zinageuzwa kuwa dawa zinazoweza kutumika kutibu magonjwa mbalimbali, badala ya kubaki kwenye machapisho ya kitaaluma.
Wito huo umetolewa leo Nov 9,2026 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, wakati wa kufungua Kongamano la Kuendeleza Sayansi katika Tiba (Advancing Science in Medical Field), lililofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo amesema tafiti na ubunifu ni muhimu katika kuongeza uwezo wa nchi kuzalisha dawa na vifaa tiba.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuimarisha mfumo wa kitaifa na mpango kazi wa kuendeleza utafiti, ugunduzi na ubia katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba, ikiwemo vinavyotokana na mimea tiba na maarifa ya tiba asilia.
Ameeleza kuwa maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele ni pamoja na ukusanyaji na uhifadhi wa maarifa ya tiba asilia, kuendeleza matokeo ya tafiti hadi kuwa bidhaa zinazoweza kuzalishwa na kutumika pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vikuu, taasisi za utafiti na viwanda.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema chuo hicho kimetenga ekari 200 kati ya ekari 400 za eneo lake kwa ajili ya kuotesha mimea inayotumika kutengeneza dawa asilia.
Amesema kupitia Taasisi ya Dawa Asili iliyopo chuoni hapo tangu miaka ya 1970, tayari wameanza kuotesha baadhi ya mimea hiyo katika bustani maalumu inayofahamika kama Botanical Garden, ambayo itasaidia kuhifadhi na kutambua aina mbalimbali za mimea tiba.
Amesema MUHAS inalenga kushirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza dawa za asili ambazo zimeonyesha uwezo wa kusaidia wagonjwa kwa kuzipeleka katika hatua zaidi za utafiti, ikiwemo majaribio ya kitabibu (clinical trials), ili kuthibitisha usalama na ufanisi wake.
Ameeleza kuwa tayari chuo hicho kimewasilisha mapendekezo kuhusu baadhi ya dawa zilizoonyesha kusaidia wagonjwa ili ziendelee kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu, kuboreshwa na kuthibitishwa kabla ya kutumika kwa upana zaidi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar, Dkt. Mayassa Salumu Ally, amesema upembuzi uliofanywa Zanzibar umebaini kuwepo kwa zaidi ya aina 300 za mimea inayotumika katika tiba asilia, huku utafiti uliofanywa takribani miaka minne iliyopita kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Berlin ukibaini kuwa asilimia 96 ya Wazanzibari hutumia tiba hiyo katika maisha yao ya kila siku.
Amesema maeneo ya Kusini Unguja, hususan Makunduchi na Kizimkazi, yana idadi kubwa ya mimea tiba pamoja na wataalamu wa tiba asilia ambao wamekuwa wakihudumia wananchi kwa kutumia maarifa waliyorithi kutoka vizazi vilivyotangulia.
Ameeleza kuwa taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na waganga wa tiba asilia kurekodi maarifa yao, dawa wanazotumia na aina za mimea ili kuhifadhi ujuzi huo, huku akitaja mmea wa Aloe Vera Pembana unaopatikana Vitongoji na Mwambe, Pemba, kuwa miongoni mwa mimea inayohitaji utafiti zaidi wa kisayansi.
Amesema kupitia ufadhili wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), taasisi hiyo imepata fedha kwa ajili ya utafiti na uendelezaji wa dawa zinazotokana na tiba asilia zinazolenga kusaidia matibabu ya kisukari, shinikizo la damu na pumu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Tanzania, Profesa Joseph Otieno, amesema kutambuliwa kwa umuhimu wa tiba asilia na Serikali, wanasayansi na hospitali kunatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya waganga wa tiba asilia na wataalamu wa kisayansi, ili kuendeleza maarifa yaliyopo kwa manufaa ya jamii.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha dawa zinazotokana na tiba asilia zinafanyiwa tafiti na kuthibitishwa kitaalamu, huku Naibu Waziri akisisitiza kuwa bidhaa zote za dawa na vifaa tiba lazima zizingatie usalama na ufanisi kabla ya kuzalishwa na kutumiwa na wananchi.

