▪ Aonya watumishi wanaodai michango ya mafuta kwa wagonjwa wa dharura
▪ Aagiza uchunguzi wa matumizi na upatikanaji wa dawa
▪ Ataka maandalizi ya barabara za Solwa yaharakishwe
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya nchini kutenga fedha za mafuta ya magari ya kubebea wagonjwa katika bajeti za huduma za afya ili wagonjwa wanaohitaji rufaa za dharura wasicheleweshwe kwa kudaiwa michango ya mafuta.
Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Novemba 9, 2026), akizungumza na wananchi wa Iselamagazi, Jimbo la Solwa, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Shinyanga.
“Tusichangishe mafuta kwenye ambulance. Ambulance ipeleke mgonjwa imharakishwe hospitalini. Ambulance sio daladala. Wala manesi wale sio makondakta wa kukusanya michango ya mafuta,” amesema.
Amemwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha magari hayo yanakuwa na mafuta na yako tayari kuhudumia wagonjwa, huku akisisitiza fedha za mafuta zitengwe kwenye bajeti zinazoandaliwa.
“Kama hamkuweka bajeti na sasa hivi mnaandaa bajeti, nataka ambulance zote ziwe standby mgonjwa ambaye anatakiwa kunusuriwa maisha yake asiombwe fedha ya mafuta,” amesema.
Aidha, amewataka wananchi wanaodaiwa michango hiyo kutoa majina yote matatu ya watumishi wanaohusika na kuelekeza watumishi wanaochelewesha huduma kwa uzembe wafukuzwe kazi badala ya kuhamishwa vituo.
Kuhusu huduma kwa wajawazito, amesema mama anayefika hospitalini akiwa na uchungu anapaswa kuhudumiwa haraka badala ya kucheleweshwa mapokezi kwa kudaiwa vifaa kama ndoo na mabeseni.
“Tusifanye mazoea kuwa sheria,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia fedha zinazotolewa kwa ajili ya dawa, kuanzia ununuzi na usambazaji hadi upatikanaji wake kwa wagonjwa.
Amesema haikubaliki kwa vituo vya afya kuripoti utoshelevu wa dawa wa zaidi ya asilimia 97, huku wagonjwa wakiendelea kuelekezwa kununua dawa kwenye maduka binafsi.
“Fedha zimekuja kiasi gani? Dawa zimenunuliwa kiasi gani? Zimekwenda wapi na wapi na wananchi wanazipataje?” amehoji.
Ameelekeza pia ununuzi wa dawa uzingatie mahitaji na aina ya magonjwa yanayojitokeza katika maeneo husika.
Kuhusu kilimo, Dkt. Mwigulu amesema kuanzia msimu ujao wa mavuno ya pamba, Serikali itaruhusu wanunuzi wengi kushiriki katika ununuzi wa zao hilo badala ya kuwa na mnunuzi mmoja katika eneo husika, ili kuongeza ushindani wa bei na manufaa kwa wakulima.
Amesema hatua hiyo inatokana na malalamiko ya wakulima aliyoyapokea akiwa mkoani Simiyu na maelekezo aliyoyatoa kwa Waziri wa Kilimo kukutana na wadau wa zao hilo.
Kuhusu barabara, amemwelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha usanifu wa barabara zilizoombewa na Mbunge wa Solwa, Ahmed Ally Salum, unahuishwa pale inapohitajika ili ziwe tayari kuzingatiwa Serikali itakapoanza miradi mipya mwaka ujao wa fedha.
Barabara hizo ni Old Shinyanga–Iselamagazi–Solwa–Salawe na Mwanangwa–Misasi–Salawe–Solwa–Kahama.
Ameeleza kuwa Serikali imeanza kuelekeza fedha za barabara, maji na umeme moja kwa moja kwenye mifuko husika ili kuharakisha utekelezaji wa miradi, huku kipaumbele cha sasa kikiwa kukamilisha miradi iliyosimama na ile ambayo mikataba yake tayari imesainiwa.
Kuhusu shughuli za kiuchumi, Waziri Mkuu amekemea utaratibu wa kushikilia pikipiki, bajaji na vitendea kazi vingine vya wananchi wanaojiajiri kutokana na makosa yanayostahili faini, akisisitiza wahusika watozwe faini kwa mujibu wa sheria bila kuzuiwa kuendelea na shughuli zao.
Aidha, amesema Serikali imechukua hatua za kuondoa kodi kwenye malighafi za kutengeneza saruji ili kusaidia kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi.
Kuhusu mgogoro wa mipaka ya hifadhi katika Jimbo la Solwa, ameahidi kufanya mawasiliano na wizara husika na kupitia mapendekezo yaliyowahi kutolewa ili kufikia uamuzi wa kudumu, huku akiwataka wananchi kuheshimu mipaka iliyopo wakati suala hilo likifanyiwa kazi.

