Aliyekuwa mweka hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Peter Mollel ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela na kulipa faini ya shilingi milioni 36 kwa kosa la wizi akiwa mtumishi wa umma.
………………………………………………………………
ALIYEKUWA mweka hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Peter Mollel na mhasibu msaidizi Ester Melkior wamehukumiwa kifungo cha miaka saba kwenda jela na kulipa faini ya shilingi milioni 36 kila mmoja kwa makosa ya wizi wakiwa mtumishi wa umma.
Kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2008 na 2010 watu hao walishirikiana kuzidisha orodha ya walipwaji mishahara ya watumishi wa halmashauri hiyo na kuwasilisha benki kisha kujipatia sh34.5 milioni.
Naibu msajili wa mahakama kuu ya Tanzania, kanda ya Arusha, John Mkwabi alisoma hukumu ya kesi hiyo namba 48/2016 juzi kwenye mahakama ya wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
Nkwabi amesema washtakiwa hao waliingiza fedha hizo sh34.5 milioni kwenye akaunti zao na kisha washtakiwa hao kuzitumia kwa manufaa yao.
Pamoja na adhabu hiyo washtakiwa hao walipigwa faini ya sh 36 milioni baada ya kutiwa hatiani kwenye makosa tisa ya matumizi ya nyaraka na kumdanganya mwajiri.
Waendesha mashataka wa Takukuru, Isdory Kyando na Adam Kilongozi waliwafikisha washtakiwa hao mahakamani hapo na kuwasomea washtakiwa hao jumla ya makosa 24.
Katika makosa hayo, 10 yalihusu kutumia nyaraka za kumdanganya mwajiri kinyume cha kifungu cha 22 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007.
Makosa 12 yalihusu wizi uliofanywa Makosa washtakiwa hao wakiwa watumishi wa umma kinyume na vifungu vya 258 na 270 vya sheria ya kanuni ya adhabu.
Makosa mawili yalihusu matumizi mabaya ya madaraka kifungu cha 31 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007.
Waendesha mashataka hao waliwasilisha ushahidi usioacha shaka mahakamani hapo kuonyesha kuwa kati mwaka 2008 na 2010 mshtakiwa wa kwanza Mollel alishirikiana na mshtakiwa wa pili Melkior kutenda makosa hayo.
Kwa pamoja walishirikiana kuzidisha orodha ya walipwaji na kiasi cha mishahara ambacho walipaswa kulipwa kwenye hati za malipo kisha kuziwakilisha nyaraka hizo benki kwa ajili ya malipo.
Kabla ya adhabu hiyo kutolewa, wakili wa utetezi Justus Ilyarugo aliiomba mahakama iwapunguzie adhabu kwani Mollel ni baba wa familia inayomtegemea na Melkior ni mama wa mtoto mmoja hana mume na mlezi wa mama yake mzazi.
Kwa upande wao, waendesha mashtaka Kyando na Kilongozi waliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa kwani makosa mabaya ili iwe fundisho kwa wengine.
Nkwabi baada ya kusikiliza hoja zilizotolewa alitoa adhabu kwa mujibu wa sheria kulingana na makosa waliyoyatenda.
Mkuu wa Takukuru wa mkoa wa Manyara, Holle Makungu alitoa wito kwa watumishi wa umma kuridhika na vipato vya haki wanavyolipwa na serikali na wenye fikra za wizi watambue Takukuru imeenea Tanzania nzima.