
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila leo Novemba 6, 2026 jijini Dar es Salaam
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, anatarajia kugawa pikipiki 564, moja kwa kila mtaa, kwa ajili ya kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Novemba 6, 2026, Chalamila amesema zoezi la ugawaji wa vyombo hivyo litaanza Novemba 14, mwaka huu, siku ambayo kutazinduliwa kampeni ya kusafisha mazingira itakayofanyika Viwanja vya Posta, Kijitonyama.
Amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kuimarisha usafi wa mazingira, kwa lengo la kuleta mabadiliko yatakayolifanya jiji la Dar es Salaam kuwa safi na lenye mazingira bora kwa wakazi wake.
Kampeni hiyo yenye kaulimbiu isemayo “Dar es Salaam safi inawezekana, tushiriki pamoja,” inalenga kuboresha uratibu na usimamizi wa shughuli za usafi katika mitaa yote 564 ya Mkoa huo.
“Jiji letu lina mitaa 564, katika tarehe hii tutagawa pikipiki moja kwa kila mtaa wa Dar es Salaam. Lengo kuu ni kuhakikisha usimamizi na uratibu wa masuala ya usafi unafanyika kwa ufanisi katika ngazi zote za jiji,” amesema.
Amefafanua kuwa pikipiki hizo zitatumiwa na watendaji wa mitaa kufanya doria, kusimamia shughuli za usafi na kuwabaini watu wanaotupa taka au kuchafua mazingira kwa makusudi, huku akisisitiza kuwa watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria baada ya kupewa elimu kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.
“Pikipiki hizi zitatumika kikamilifu na watendaji wa mitaa kufanya doria, uratibu wa usafi na kuwabaini watu wote wanaochafua mazingira kwa makusudi, ambao mbali na kupewa elimu, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” amesisitiza.
Aidha, amesema Serikali ya Mkoa imefanikiwa kupata mwekezaji kutoka nchini Ghana ambaye anatarajia kujenga kiwanda katika Dampo la Pugu kwa ajili ya kuchakata taka na kuzalisha mbolea pamoja na bidhaa nyingine, ikiwemo nishati. Hatua hiyo inatarajiwa kusaidia kupunguza kiasi cha taka na kuimarisha usafi katika maeneo ya makazi.
Katika hatua nyingine, ameeleza kuwa Mkoa unaandaa mpango mpya wa maendeleo ya jiji, unaohusisha pia mapendekezo ya kuhamisha kata 10 za Manispaa ya Temeke ili kupisha upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Amesema wataalamu kutoka Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam wanatarajiwa kukutana na Wizara ya Ujenzi kuwasilisha andiko la ujenzi wa barabara itakayounganisha Kisarawe na Chaliwe, kwa lengo la kurahisisha usafiri wa malori, huku magari madogo yakitumia Barabara ya Morogoro.
Kwa mujibu wa Chalamila, mpango huo unalenga kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, hususan katika njia zinazotumiwa na magari makubwa yanayoelekea bandarini.
Akizungumzia upande wa michezo, amesema anatarajia kwenda nchini Qatar kuishangilia timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, itakayoshiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika kuanzia Novemba 19 hadi Desemba 13, 2026.
Amesema mbali na yeye kushiriki katika kutoa hamasa kwa vijana hao, pia kuna mpango wa kugharamia safari ya baadhi ya mashabiki wa Tanzania watakaopata nafasi ya kwenda Qatar kushuhudia na kuishangilia timu hiyo.
Amewataka Watanzania kuungana na Serikali kuiunga mkono Serengeti Boys, akieleza kuwa kufuzu kwa timu hiyo kushiriki mashindano hayo ni hatua kubwa na ya kujivunia katika maendeleo ya soka la vijana nchini.
Amesema ushiriki wa vijana hao katika mashindano hayo ya kimataifa unapaswa kuwaunganisha Watanzania bila kujali tofauti zao, kwa kuwa wanaiwakilisha nchi katika jukwaa kubwa la soka duniani.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo ni miongoni mwa matunda ya uwekezaji unaofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya michezo, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kutoa hamasa kwa timu hiyo ili iweze kufanya vizuri na kuipeperusha vyema bendera ya taifa.
Ameongeza kuwa sapoti ya mashabiki ni sehemu muhimu ya kujenga morali kwa wachezaji wanapojiandaa kukabiliana na wapinzani wao katika michuano hiyo ya kihistoria.
