Na Silivia Amandius Missenyi, Kagera.
Katika kuimarisha ushiriki wa vijana na wanawake katika sekta ya kilimo, Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 395 katika Shamba la Kyakakela, Kijiji cha Kashaba, Kata ya Kyaka, kwa ajili ya utekelezaji wa programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT).
Programu hiyo inalenga kuwawezesha vijana na wanawake 278 kushiriki katika kilimo cha kibiashara, kupata fursa za ajira na kuongeza kipato kupitia shughuli za uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shamba hilo, Mratibu wa Programu ya BBT Wilaya ya Missenyi, Bw. Edwin King Edward, amesema programu hiyo imekusudiwa kuwajengea wanufaika uwezo wa kujiajiri, kuajiri wengine na kuchangia maendeleo ya kiuchumi.
Amesema kila Halmashauri inayotekeleza programu hiyo inapaswa kuwa na eneo la kilimo cha pamoja kwa ajili ya wanufaika, huku akieleza kuwa shamba hilo limeandaliwa kwa ajili ya kilimo cha zao la mpunga kupitia ushirikiano na Wizara ya Kilimo.
Aidha, amesema hatua za awali za maandalizi zimeanza kwa kulisafisha shamba na kulima hatua, sambamba na utoaji wa mbegu kwa ajili ya uzalishaji. Wanufaika wanatarajiwa kuendeleza shughuli hizo baada ya kupata ujuzi na maarifa yanayohitajika.
Kwa mujibu wa Mratibu huyo, Halmashauri kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo imeandaa mafunzo ya nadharia na vitendo yatakayodumu kwa miezi miwili, kuanzia Novemba 6, 2026 hadi Januari 6, 2027, yakilenga kuwajengea wanufaika uwezo wa kusimamia na kuendesha shughuli za kilimo kwa kuzingatia utaalamu na teknolojia za kisasa.
Kwa upande wake, Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Mhe. Kanal Isaac Anthony Mwakisu, amewapongeza vijana na wanawake waliochaguliwa kunufaika na programu hiyo na kuwataka kuzingatia nidhamu, uwajibikaji pamoja na maelekezo ya wataalamu katika kutekeleza majukumu yao.

