Kamishna Hussein Mbaga, aliyemwakilisha Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo akifungua mkutano huo jijini Arusha

Kamishna Msaidizi Ustawi na Mwitikio wa Jamii DCEA, Sarah Ndaba akizungumza kwenye mkutano huo jijini Arusha

Naye Msimamizi wa PTACC Africa, Dkt. Yvonne Olando akizungumza kwenye mkutano huo jijini Arusha

………..
Na Happy Lazaro, Arusha.
Arusha .Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema inaendelea kuboresha mikakati ya kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya nchini kwa kuweka kipaumbele katika matibabu, ustawi wa waathirika na kulinda utu wa binadamu badala ya kutegemea mfumo wa adhabu za jinai pekee.
Akifungua mkutano wa PTACC Africa Defrection Summit, Kamishna Hussein Mbaga, aliyemwakilisha Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema mamlaka hiyo imejipanga kuendana na mifumo ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na dawa za kulevya na uhalifu (UNODC) pamoja na Rome Consensus.
Amesema wajibu mkubwa wa mamlaka hiyo ni kulinda maisha, kupunguza mateso na kuheshimu utu wa binadamu, huku akieleza kuwa Tanzania ina nafasi ya kuwa mfano wa kuigwa katika eneo hilo kutokana na kuendelea kuboresha mkakati wa kitaifa unaoweka afya ya binadamu kuwa kipaumbele sambamba na usalama wa jamii.
Mbaga amesema watu wanaokabiliwa na utegemezi mkubwa wa dawa za kulevya wanapaswa kutambuliwa kama wagonjwa wanaohitaji huduma za kitabibu, msaada wa kisaikolojia na fursa ya kurejea katika maisha ya kawaida badala ya kukabiliwa na hatua za mfumo wa haki jinai pekee.
“Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, Tanzania imepiga hatua katika kuunganisha huduma za afya ya jamii na usalama wa taifa kupitia ushirikiano wa DCEA, Wizara ya Afya na wadau mbalimbali, hatua iliyowezesha kupanua huduma za matibabu ya MAT na kliniki za OAT katika maeneo mbalimbali nchini.”amesema Mbaga .
Ameongeza kuwa kwa sasa maelfu ya Watanzania wanapata huduma ya matibabu ya methadone kila siku, inayosaidia kuokoa maisha yao, kuwajengea uwezo wa kurejea kazini, kujenga upya maisha na kuungana tena na familia zao.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Ustawi na Mwitikio wa Jamii DCEA, Sarah Ndaba, amesema mkutano huo wa siku mbili umewakutanisha wadau zaidi ya 100 kutoka maeneo mbalimbali kwa lengo la kujadili namna ya kuwasaidia waraibu wanaojikuta katika migogoro na sheria kupata matibabu badala ya kupelekwa moja kwa moja kwenye mfumo wa adhabu.
Amesema uraibu unaweza kumfanya mtu kujihusisha na vitendo mbalimbali ili kupata fedha za kununulia dawa za kulevya, hivyo ni muhimu kutafuta suluhisho linalolenga kumsaidia kuondokana na utegemezi huo.
Naye Msimamizi wa PTACC Africa, Dkt. Yvonne Olando, amesema mpango wa Deflection unalenga kuwaunganisha polisi, mashirika ya kiraia, madaktari na wanasaikolojia ili kuwasaidia watu wenye changamoto za matumizi ya dawa za kulevya na afya ya akili kupata huduma stahiki badala ya kuishia katika mfumo wa haki jinai.
Amesema mfumo huo unahitaji kuwekwa rasmi ili polisi wanapomwelekeza mtu mwenye uraibu kupata matibabu wasitafsiriwe vibaya kuwa wamehongwa au wanapendelea watuhumiwa. Ameongeza kuwa mafunzo ya pamoja kwa polisi na wataalamu wa afya ni muhimu ili kuhakikisha wanaohitaji msaada wanapelekwa hospitalini na kupata matibabu yanayostahili.
Kwa upande wake, DCP Naibu Kamishna wa polisi ,Henry Mwaibambe , amesema jeshi hilo limekuwa likitekeleza miradi mbalimbali ya usalama wa jamii, ikiwemo Polisi Kata katika kata 3,956 za Tanzania Bara na shehia 358 za Zanzibar, inayosaidia kutambua na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Amesema baadhi ya waraibu wanapowekwa pamoja na watuhumiwa wengine kwenye mahabusu au magerezani wanaweza kukumbana na vitendo vya udhalilishaji kutokana na hali zao za kiafya, hivyo mfumo wa Deflection utasaidia kuwapatia huduma zinazolingana na mahitaji yao.
Ameongeza kuwa kupitia mpango wa Familia Yangu Haina Uhalifu, jamii inapaswa kutoa taarifa mapema kuhusu viashiria vya uraibu, badala ya kuwatenga waathirika, ili waweze kupata matibabu na kurejea katika maisha ya kawaida.
