Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imesema inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa katika vituo vya afya nchini, ikiwemo Kituo cha Afya Kintinku kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Martha Nehemia Gwau, aliyetaka kujua lini Serikali itajenga wodi za wagonjwa katika kituo hicho.

Akijibu swali hilo, Profesa Shemdoe amesema Kituo cha Afya Kintinku kilipokea Sh milioni 500 mwaka 2017/18 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma za afya.

Amesema fedha hizo zilitumika kujenga jengo la wazazi, jengo la upasuaji, maabara, jengo la kufulia, jengo la kuhifadhia maiti pamoja na nyumba ya mtumishi.

Ameeleza kuwa majengo hayo yamekamilika na yanaendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Aidha, amesema Serikali inatekeleza ujenzi wa miundombinu katika vituo vya afya kwa awamu, ambapo kipaumbele cha awali kilikuwa ujenzi wa wodi za uzazi na majengo ya upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito.

Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa katika vituo vya afya, ikiwemo Kituo cha Afya Kintinku, ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.