Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Novemba 4, 2026, ameshiriki zoezi la kupiga kura katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Chamwino, akipiga kura katika Kituo cha Ofisi ya Kijiji cha Chamwino, mkoani Dodoma.

Uchaguzi huo unafanyika kufuatia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chamwino, Deogratius Ndejembi, kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kuhitajika kumpata mwakilishi mpya wa wananchi wa jimbo hilo.

Wakizungumza baada ya kushiriki uchaguzi huo, baadhi ya wananchi waliojitokeza kupiga kura wameeleza kuridhishwa na namna zoezi lilivyoendeshwa, wakisema wamefurahishwa na maandalizi pamoja na huduma zilizotolewa katika vituo vya kupigia kura.

Mchungaji Nyembela, mkazi wa Chamwino, amesema amefurahishwa na maandalizi ya uchaguzi huo, huku akiwataka vijana kupenda nchi yao, kuheshimu viongozi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Paulina George Mkasanga, mkazi wa Kata ya Chamwino Mkuu na Mwenyekiti wa Shina Namba Moja, amesema zoezi limekuwa zuri na lenye uwazi, huku akiwahimiza wananchi ambao hawajapiga kura kujitokeza kushiriki katika uchaguzi huo.

Naye Doris Wilson Doroji amesema ameridhishwa na namna zoezi lilivyoendeshwa, akieleza kuwa wazee wamekuwa wakipatiwa msaada wanapofika vituoni, ikiwemo kushikwa mkono na kuelekezwa maeneo sahihi ya kupigia kura.

Aidha, baadhi ya wazee walioshiriki uchaguzi huo wamesisitiza umuhimu wa wananchi kuchagua viongozi wanaowaamini, wakieleza kuwa viongozi wanaochaguliwa ndio wanaowasilisha changamoto na mahitaji ya wananchi katika ngazi mbalimbali za maamuzi.

Wamesema pia uchaguzi huo umefanyika katika mazingira ya amani, huku wakitoa wito kwa vijana kujitokeza kushiriki katika uchaguzi na kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu katika jamii.

Kwa mujibu wa takwimu za uchaguzi, jumla ya wapiga kura 213,024 wameandikishwa kushiriki uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Chamwino na Udiwani katika kata 11 za Tanzania Bara. Kati yao, wapiga kura 133,864 wapo Jimbo la Chamwino na 79,160 katika kata hizo 11.

Katika uchaguzi huo, jumla ya vituo 665 vya kupigia kura vinatumika, ambapo vituo 441 vipo Jimbo la Chamwino na vituo 224 vipo katika kata 11 zinazofanya uchaguzi mdogo.