Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma 

Naibu  Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, amesema asilimia 70 ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo inategemea ushiriki wa sekta binafsi, hivyo ukuaji wa uchumi wa nchi unahitaji ushiriki dhabiti wa sekta hiyo.

Akizungumza Novemba 3, 2026 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Maendeleo ya Viwanda nchini kuelekea uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025, Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Mwaka 2003, Toleo la Mwaka 2025, pamoja na uzinduzi wa Programu ya Ushirikiano wa Nchi (PCP), Londo amesema sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo.

Amesema kuwa wakati wa kubinafsisha mashirika ya umma, iliaminika kuwa kuondoa serikali katika uendeshaji wa mashirika hayo na kuyaweka chini ya sekta binafsi, ikiwemo viwanda na rasilimali muhimu, kungewezesha kukuza mauzo ya bidhaa nje ya nchi pamoja na kuongeza uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya matumizi ya ndani.

Aidha amebainisha kuwa kupitia kongamano hilo, wadau wanapaswa kujadili kwa mapana Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2020–2050 na namna bora ya kuitafsiri katika hatua halisi za kuongeza uwekezaji na uzalishaji wa viwanda, kuongeza thamani ya mazao na kujenga uchumi unaotumia rasilimali za ndani kuzalisha bidhaa zenye thamani kubwa.

Pia ameongeza kuwa kuna umuhimu wa kuacha kuendelea kuuza malighafi nje ya nchi na kuagiza bidhaa ambazo zina uwezo wa kuzalishwa ndani ya nchi.

Amesema kuwa katika kuimarisha maendeleo ya viwanda nchini, Serikali imeandaa Sera ya Maendeleo ya Viwanda ya Mwaka 2025 ambayo itatambulishwa kwa wadau katika kongamano hilo.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum, amesema kuwa kupitia Programu ya Ushirikiano wa Nchi (PCP), wanatarajia kuimarisha uratibu wa miradi na programu za maendeleo ya viwanda, kuongeza thamani ya malighafi, kukuza ujuzi, kuvutia uwekezaji, kuongeza mauzo ya nje na kuendeleza uzalishaji unaozingatia utunzaji wa mazingira.

Ameongeza kuwa kongamano hilo linatarajiwa kupata maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu hatua za kuondoa vikwazo vya uwekezaji na uzalishaji, kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani na kubainisha miradi ya kipaumbele inayoweza kutekelezwa kupitia ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo

uzinduzi unatarajia kufanyika kesho Novemba 4,2026 na Mgeni Rasmi anatarajiwa Kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.