Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kazi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) itapimwa kwa matokeo yanayoonekana, huku akisisitiza kuwa bunifu zinazofanywa nchini zinapaswa kufikia hatua ya kuwa bidhaa zinazotumika na kununuliwa na wananchi.Akizungumza Novemba 3, 2026 jijini Dodoma wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la jengo la COSTECH, Prof. Mkenda amesema bunifu zinazowasilishwa katika maonyesho zinapaswa kuingia sokoni na kutatua changamoto za wananchi, badala ya kubaki kuwa bunifu za maonyesho kila mwaka.

Amesema kuwa COSTECH, Kurugenzi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STI), vyuo vikuu na wadau wengine wanapaswa kuhakikisha tafiti zinafanyika, matokeo yanapatikana na yanatumika kutatua changamoto mbalimbali za wananchi.

Aidha, amebainisha kuwa COSTECH ina jukumu la kuratibu masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu nchini kote, ikiwemo kuhakikisha matokeo ya tafiti yanafahamika na kutumiwa na wizara na wadau wanaohusika.

Amesema kuwa mfano wa utafiti uliofanywa na Profesa Ndakidemi kuhusu matumizi ya mbolea na umwagiliaji unapaswa kuratibiwa na COSTECH ili matokeo yake yawafikie wadau wa kilimo na kuwanufaisha wananchi.

Pia ameongeza kuwa COSTECH, NIMR na taasisi nyingine zinapaswa kushirikiana na wizara zinazohusika kuhakikisha tafiti, ikiwemo pre-clinical trial, zinafanyika na kuwekwa kwenye bajeti ili sayansi iweze kutoa majibu ya uhakika kuhusu matumizi na madhara ya teknolojia au tiba zinazobuniwa.

Prof. Mkenda amesema kuwa ujenzi wa jengo, utoaji wa ufadhili wa masomo na hatua nyingine ni mchakato, lakini matokeo yanayotarajiwa ni kuona sayansi na teknolojia zikigusa na kuboresha maisha ya wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema ujenzi wa jengo hilo ulianza Machi 2025 na umefikia asilimia 99, huku ujenzi mzima ukigharimu Sh bilioni 10.26.

Amebainisha kuwa kati ya fedha hizo, Sh milioni 565.5 zimetumika kwa usanifu na usimamizi wa ujenzi, huku Sh bilioni 9.795 zikitolewa kwa mkandarasi kwa ajili ya ujenzi pamoja na mifumo mbalimbali, ikiwemo umeme wa TANESCO, jenereta, lifti, mfumo wa kiyoyozi, ulinzi wa moto, maji safi ya DUWASA na kisima.

Pia ameongeza kuwa jengo hilo lina matanki 18 ya kuhifadhi maji yaliyopo juu ya jengo na matanki 120 yaliyopo chini ya ardhi.