Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umetaja changamoto ya gharama za uendeshaji na upatikanaji wa utaratibu endelevu wa kugharamia huduma za intaneti ya bure (Public WiFi) katika maeneo ya wazi kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyoathiri upanuzi wa huduma hiyo nchini.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwenye kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina leo Novemba 3, 2026, Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa UCSAF, Albert Richard, amesema mfuko huo umeanza kutekeleza mpango wa kupeleka huduma za WiFi katika maeneo ya wazi, lakini changamoto kubwa imekuwa namna ya kugharamia huduma hizo baada ya kukamilika kwa uwekaji wa miundombinu.

Amesema changamoto hiyo hujitokeza zaidi baada ya kukamilika kwa hatua ya kwanza ya mradi, ambapo taasisi zinazohusika zinapaswa kuendeleza huduma na kugharamia matumizi ya kila siku, jambo ambalo limekuwa likihitaji utaratibu maalumu.

Richard amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 mfuko ulianzisha mradi huo kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa intaneti katika maeneo ya wazi, huku katika mwaka wa fedha 2025/26 ukiwa na mpango wa kufikisha huduma hiyo katika maeneo 60 Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema mfuko huo unaendelea kutafuta mfumo utakaowezesha wananchi kupata huduma hiyo kwa urahisi na kwa gharama nafuu, ikiwemo utaratibu wa kuwapatia watumiaji muda wa awali wa intaneti bila malipo kabla ya kuendelea na huduma kwa malipo.

Alieleza kuwa mfumo huo unalenga kuongeza matumizi ya teknolojia na kuwapa wananchi fursa ya kupata taarifa, kufanya shughuli mbalimbali za kidijitali na kuwasiliana kwa urahisi.

Pamoja na changamoto hizo, Richard amesema UCSAF inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya upanuzi wa huduma za mawasiliano ya simu nchini, kupitia ujenzi wa minara katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara, ili kuhakikisha wananchi wanaoishi maeneo hayo wanapata huduma za mawasiliano kwa uhakika.

Amesema kufikia Septemba 2026, UCSAF imeingia mikataba na watoa huduma za mawasiliano kwa ajili ya kufikisha huduma katika kata 2,306 zenye vijiji 5,505 nchini, kupitia ujenzi wa jumla ya minara 2,324. Kukamilika kwa miradi hiyo kunatarajiwa kuwezesha zaidi ya wananchi 32,789,590 kupata huduma za mawasiliano ya simu kwa uhakika.

Richard amesema hadi kufikia kipindi hicho, huduma za mawasiliano zimefika katika kata 2,053 zenye vijiji 5,185, ambapo jumla ya wananchi 30,051,214 tayari wamenufaika kupitia ujenzi wa minara 2,199.

Aidha, amesema utekelezaji wa miradi hiyo bado unaendelea katika kata 253 zenye vijiji 320, ambako minara 251 inajengwa kwa lengo la kuwafikia wananchi 2,973,121 na kuwaunganisha na huduma za mawasiliano. Alisema gharama za utekelezaji wa miradi hiyo ya upanuzi wa mawasiliano zinafikia jumla ya shilingi bilioni 374.

Amesema tangu mwaka 2012, UCSAF imeingia mikataba ya ujenzi wa minara 2,324 katika awamu 21, huku minara 2,199 ikiwa imekamilika, hatua iliyochangia kupanua huduma za mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini.

Richard alisema pia mradi wa ujenzi wa minara 758 uliotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 126 umekamilika na kufanikiwa kuwafikishia huduma za mawasiliano wananchi wapatao milioni 8.5.

Alisema mfuko huo unaendelea na mradi mwingine wa ujenzi wa minara 287 kwa gharama ya shilingi bilioni 29, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za mawasiliano.

Aliongeza kuwa UCSAF pia inashughulikia changamoto ya mawasiliano katika reli ya kisasa ya SGR, kwa kuandaa mpango wa kuhakikisha abiria wanapata huduma za mitandao mbalimbali wanaposafiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma.

Katika sekta ya utangazaji, Richard alisema mfuko huo unaendelea kuboresha usikivu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupitia ujenzi wa vituo 37 vya matangazo kwa gharama ya shilingi bilioni 15.5, huku baadhi vikiwa vimekamilika na vingine vikiendelea kutekelezwa.

Alisema pia zaidi ya maeneo 15 yamehusishwa katika mradi wa redio za jamii unaojumuisha ujenzi wa minara na studio kwa gharama ya shilingi bilioni sita, ili kuongeza upatikanaji wa taarifa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali.

Kuhusu elimu, Richard amesema zaidi ya shule 1,167 zimefaidika na mradi wa usambazaji wa vifaa vya TEHAMA kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 17.7, huku shule 22 zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu zikipatiwa vifaa vinavyowasaidia kupata elimu ya kidijitali.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Msajili wa Hazina, Sabatho Kosuli, amesema UCSAF inapaswa kutazamwa kama taasisi ya kimkakati katika kukuza uchumi na maendeleo ya jamii, kwa kuwa huduma za mawasiliano zinafungua fursa za ajira, biashara na uchumi wa kidijitali.

Amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 unahitaji uchumi wa kisasa unaotegemea teknolojia, hivyo akawataka waandishi wa habari kuelimisha wananchi kuhusu miradi inayotekelezwa na fursa zinazotokana na upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini.