Na Mwandishi wetu, Simanjiro 

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Mkoani Manyara, wamemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, kuwezesha miji midogo ya Mirerani na Orkesumet ili wafanye vikao.

Madiwani hao wamepitisha azimio hilo kwenye kikao chao kilichofanyika makao makuu ya Wilaya hiyo mji mdogo wa Orkesumet.

Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii, Albert Msole amesema miji midogo ya Mirerani na Orkesumet inapaswa kuwezeshwa ili wajumbe wake waweze kukutana kujadili na kupitisha maendeleo yao.

“Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri awezeshe mamlaka ya miji midogo ya Orkesumet na Mirerani ili ziweze kujiendesha na kufanya vikao kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Pia, baraza hilo la madiwani limemuagiza Mkurugenzi aweke kwenye bajeti mpango wa kujenga ofisi na nyumba za watumishi wa ngazi ya vijiji na kata.

Amesema Mkurugenzi mtendaji wa Wilaya afuatilie wawekezaji mbalimbali Wilayani ili kuwezesha Halmashauri kupata fedha kutokana na michango ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) iliyopo kwa mujibu wa sheria.

“Pia Mkurugenzi mtendaji aweke kwenye bajeti ijayo ujenzi wa zahanati kwenye vijiji ambavyo hazina zahanati,” amesema Msole.

Amesema Mkurugenzi mtendaji aweke mkakati wa kuondoa tatizo la upungufu wa madarasa na madawati katika shule ya msingi na sekondari.

“Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri aendelee kuagiza watendaji wa kata na vijiji watunge sheria ndogo zinazowataka wazazi kuchangia chakula cha mchana cha wanafunzi na rasimu ya sheria hiyo ipitishwe kwenye mikutano mikuu ya vijiji, zoezi hilo liwe limekamilika mwishoni mwa mwezi Novemba 2026,” amesema.

Amesema Mkurugenzi mtendaji awaagize watendaji wa Kata na Vijiji kuendelea kuweka mikakati ya kujenga miundombinu mbalimbali kwa kuzingatia upungufu ikiwa pamoja na ujenzi wa shule mpya kwenye Kata na Vijiji vyenye uhitaji wa shule za sekondari ili kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza Januari 2028.

Ameeleza kwamba pia, Mkurugenzi mtendaji anapaswa kuweka mikakati ya kukamilisha ujenzi wa maabara za shule za sekondari ambao ujenzi wake ulianza muda mrefu na hazijakamilika.