NA Denis Mlowe, Iringa

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekabidhi kompyuta 20, mashine ya kurudufu nyaraka (fotokopi), printa na vifaa vingine kwa Klabu ya Kodi ya Shule ya Sekondari Tosamaganga mkoani Iringa, kwa lengo la kuimarisha elimu ya kodi na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) miongoni mwa wanafunzi.

Vifaa hivyo vimekabidhiwa na Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Maigloria Saria, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyolenga kutekeleza ahadi iliyotolewa na mamlaka hiyo Oktoba 10, mwaka huu, wakati wa maadhimisho ya miaka 100 ya Shule ya Sekondari Tosamaganga.

Akizungumza katika hafla hiyo, Saria ameupongeza uongozi wa shule, walimu, wanafunzi na wadau wengine kwa ushirikiano wao katika kuanzisha na kuendeleza Klabu ya Kodi, akisisitiza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuboresha ujifunzaji na kuwajengea wanafunzi uelewa wa masuala ya kodi.

Pia, amemshukuru Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuf Juma Mwenda, kwa mchango wake katika kufanikisha upatikanaji wa fedha za kununua vifaa hivyo baada ya ofisi ya TRA Mkoa wa Iringa kuwasilisha mahitaji ya klabu hiyo. 

Amesema Kamishna Mkuu Mwenda ana uhusiano wa pekee na shule hiyo kwa kuwa ni mmoja wa wahitimu wake na kusema kuwa matumizi ya teknolojia ni sehemu muhimu ya maendeleo ya elimu na uchumi, hivyo kompyuta hizo zitawasaidia wanafunzi kujifunza matumizi sahihi ya TEHAMA, kufanya tafiti, kuandaa kazi za kitaaluma na kukuza ubunifu utakaowasaidia katika maisha yao ya sasa na baadaye.

Ameongeza kuwa Klabu ya Kodi inapaswa kuwa kitovu cha elimu ya kodi shuleni na katika jamii, kwa kuwafundisha wanafunzi haki na wajibu wa walipakodi, umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati na mchango wa mapato ya serikali katika kugharamia huduma za kijamii na maendeleo ya taifa.

Amewataka wanachama wa klabu hiyo kutumia maarifa wanayopata kuwaelimisha wanafunzi wenzao, wazazi, ndugu na jamii inayowazunguka kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari, akibainisha kuwa kodi huchangia kugharamia huduma muhimu zikiwemo elimu, afya, maji na ujenzi wa barabara.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Tosamaganga, Laurent Manga, ameishukuru TRA kwa msaada huo, akisema klabu hiyo imekuwa hai na ina mchango mkubwa katika kuwajengea wanafunzi uelewa wa masuala ya kodi kwani elimu hiyo ni muhimu kwa kuwa wanafunzi hao ni walipakodi wa sasa na wa baadaye.

Manga amesema wanafunzi wana nafasi kubwa ya kueneza elimu ya kodi nje ya mazingira ya shule kwa kuwafikishia wazazi, ndugu na jamii ujumbe kuhusu umuhimu wa kodi katika maisha ya kila siku. 

Amesema kuwa hata huduma zinazotolewa na serikali pamoja na baadhi ya mahitaji yanayotumika shuleni hutegemea mapato yanayotokana na kodi. 

Manga alisema kuwa Klabu ya Kodi ilianzishwa Novemba 2025 na kuzinduliwa rasmi Machi 14, 2026, ikiwa na wanachama 230 na kufanya kazi kwa Kupitia mikutano na shughuli mbalimbali za kielimu, klabu hiyo imeendelea kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari na kueleza mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa.

Mkuu wa shule Manga alisema anashukuru kwa kukabidhiwa kompyuta 20, fulana 270 kwa wanachama wa klabu na wafanyakazi wa shule, printa moja, mashine moja ya fotokopi, pamoja na vitabu na machapisho ya elimu ya kodi kuongeza kuwa viifaa hivyo vinatarajiwa kurahisisha shughuli za kielimu, uchapishaji wa nyaraka na uenezaji wa elimu ya kodi kwa wanafunzi na jamii.

Naye Mratibu wa Klabu za Kodi za TRA nchini, Hudson Kamoga, amesema msaada huo una umuhimu mkubwa zaidi ya thamani ya vifaa vyenyewe, kwa kuwa unalenga kujenga maarifa, uelewa na mtazamo chanya kuhusu kodi miongoni mwa vijana. 

Amesema TRA inaamini kuwa utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari unapaswa kujengwa mapema kabla vijana hawajaingia katika ajira, biashara na uwekezaji.

Kamoga amesema TRA inaendelea kuimarisha klabu za kodi katika shule na taasisi za elimu ya juu nchini ili kuandaa kizazi kitakachotambua wajibu wake katika kuchangia maendeleo ya taifa. 

Amewahimiza wanafunzi kuuliza maswali, kushiriki mijadala, kuandika insha na kutumia maarifa wanayopata kuwa mabalozi wa elimu ya kodi katika familia na jamii zao na kusisitiza kuwa lengo la TRA si kujenga taifa ambalo wananchi wanalipa kodi kwa kuogopa adhabu, bali ni kujenga kizazi kinachoelewa umuhimu wa kodi na kinachojivunia kutimiza wajibu huo kwa hiari. 

Ameongeza kuwa klabu hiyo inatarajiwa kuwa miongoni mwa klabu za mfano nchini katika kuhamasisha uwajibikaji na uelewa wa masuala ya kodi.

Kwa upande wao, wanachama wa Klabu ya Kodi ya Tosamaganga wameahidi kutunza vifaa vilivyokabidhiwa na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na wataendelea kujifunza sheria na taratibu za kodi, kueneza elimu hiyo kwa wanafunzi wenzao na jamii, pamoja na kuhamasisha ulipaji kodi kwa wakati, kurasimisha biashara na kudai risiti za manunuzi.