Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile akifungua Mafunzo juu ya ugonjwa wa Corona kwa watoa huduma za afya kutoka katika vituo vya afya halmashauri ya wilaya ya Ushetu,Kahama Mji na Msalala yaliyofadhiliwa na Shirika la LifeWater International leo Alhamis Mei 7,2020 kwenye Ukumbi wa Kahama College of Health Sciences mjini Kahama. Picha zote na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile akiwasisitiza wataalamu wa afya kutumia taaluma yao vizuri ili kuokoa maisha ya Watanzania huku akiwataka kuondoa hofu,wasiwasi na mashaka akisisitiza kuwa kitendo cha mtu kuwa na dalili za Corona kisimnyime haki ya kutibiwa magonjwa mengine.
Watoa huduma za afya kutoka kwenye vituo vya afya wilayani Kahama wakimsikiliza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile.
Meneja wa Shirika la LifeWater International Mkoa wa Shinyanga,Benety Malima akizungumza wakati wa Mafunzo juu ya ugonjwa wa Corona kwa watoa huduma za afya 43 kutoka katika vituo vya afya vya serikali na watu binafsi wilayani Kahama ‘halmashauri ya wilaya ya Ushetu,Kahama Mji na Msalala’ ambapo alisema wameamua kushirikiana na serikali kutoa mafunzo ya COVID 19 kwa watoa hudumza a afya kwa sababu wapo mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya COVID 19.
Watoa huduma za afya katika vituo vya afya wilayani Kahama wakiwa ukumbini.
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile amewashauri watumishi wa sekta ya afya kutumia taaluma zao vizuri kuwa na ujasiri na moyo wa kulitumikia taifa katika kipindi hiki cha Janga la Corona huku akisisitiza kuwa siyo kila mgonjwa mwenye dalili za Corona na ana Corona hivyo asinyimwe haki ya kutibiwa magonjwa mengine.
Dkt. Ndungile ameyasema hayo leo Alhamis Mei 7,2020 wakati akifungua Mafunzo juu ya ugonjwa wa Corona kwa watoa huduma za afya 43 kutoka katika vituo vya afya vya serikali na watu binafsi wilayani Kahama ‘halmashauri ya wilaya ya Ushetu,Kahama Mji na Msalala’ yaliyofadhiliwa na Shirika la LifeWater International linalojihusisha na masuala ya Upatikanaji wa Maji Safi na Salama,Afya na Usafi wa Mazingira.
Alisema katika janga hili la Corona matumaini ya Watanzania yapo kwa watumishi wa sekta ya afya hivyo msingi mkubwa ni kutoa matibabu sahihi kwa mgonjwa bila kujali rangi,kabila ,dini ,uwezo wake ama mahali anapotoka ili kuzuia vifo visivyokuwa vya lazima.
“Sisi watumishi wa afya ni sawa na pale inapotokea vita matumaini ya wananchi yanakuwa kwa askari. Kwenye janga hili la Corona sisi ndiyo kimbilio. Tunatakiwa kuwa na ujasiri na moyo wa kulitumikia taifa letu. Hatutarajii mtu amekuja kwenye kimbilio halafu na wewe unamkimbia au unamnyima huduma stahiki au unamtenga au unamnyanyapaa kwa sababu umehisi ana Corona”,alisema Dkt. Ndungile.
Aliwataka wataalamu wa afya kutumia taaluma yao vizuri ili kuokoa maisha ya Watanzania huku akiwataka kuondoa hofu,wasiwasi na mashaka akisisitiza kuwa kitendo cha mtu kuwa na dalili za Corona kisimnyime haki ya kutibiwa magonjwa mengine.
“Kuna wagonjwa wengine watakuja na magonjwa mengine tofauti na Corona. Historia ya mgonjwa ichukuliwe kwa mujibu wa taratibu za kitabibu,huenda mtu ana homa,anakohoa, ana kifua Kikuu,Maleria, shinikizo la damu,tatizo la moyo,Kisukari, Aleji, Pumu, HIV nk. Kwa hiyo lazima tutambue kuwa mgonjwa atatibiwa kwa ujumla wake na siyo tu kuangalia kipengele cha Corona”,alieleza Dkt. Ndungile.
“Niwaombe sana wataalamu tusiwanyanyapae wagonjwa maana unaweza kuzuka mtindo..Hivi wewe umetokea wapi? Dar wiki mbili zilizopita..Aaah! kaa huko kwenye hicho chumba! Na pengine anaweza tu akawa na hofu kuwa ana Corona…Yaani wewe hujachukua hata historia ya mgonjwa,hata vipimo tayari wewe unamtenga,halafu humpi huduma yoyote akisubiri mpaka vipimo vya Corona”,alisema Dkt. Ndungile.
“Kuna mwingine unakuta ana pumu, mwingine matatizo tu ya presha,hajatumia dawa,presha imepanda na presha ikiwa juu sana mtu anaweza kubanwa na kifua,mbavu na wakati mwingine vichomi, Sasa wewe ukisikia tu mbavu zinauma unasema hii ni Corona halafu unamfungia hapo unasubiri hadi DMO akupe maelekezo matokeo yake mtu anapoteza maisha”,aliongeza Dkt. Ndungile.
Mganga huyo wa Mkoa alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo juu ya Corona kwa watoa huduma za afya mkoani Shinyanga ili wawe na uelewa mzuri kuhusu namna ya kutambua na kubaini mgonjwa wa Corona,kutoa matibabu sahihi kwa wagonjwa,namna ya kuzuia maambukizi yasienee na kujilinda wasipate maambukizi.
“Ninalishukuru Shirika la LifeWater International kwa kuwezesha mafunzo haya ya Corona kwa watoa huduma za afya mkoani Shinyanga.Tayari tumetoa mafunzo kama haya katika halmashauri ya Shinyanga,Manispaa ya Shinyanga na Kishapu na kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama Mji, Msalala na Ushetu mafunzo yanafanyika leo na kesho”,alisema Dkt. Ndungile.
Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la LifeWater International Mkoa wa Shinyanga, Benety Malima alisema wameamua kushirikiana na serikali kutoa mafunzo ya COVID -19 kwa watoa hudumza a afya kwa sababu wapo mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya COVID- 19.
“Tumeona nyinyi ni watu muhimu sana ambao mnatakiwa kupata mafunzo haya na mkayafanyie kazi kwa kujilinda nyinyi wenyewe na kusaidia wale mnaowahudumia. Bila wataalamu wa afya pengine tunaweza kuwa na tatizo kubwa sana la COVID -19”,alisema Malima.
“Nyinyi ndiyo mnakutana na wagonjwa,nyinyi ndiyo mnakutana na washukiwa kwa hiyo msipokuwa na uelewa mpana kuhusu COVID 19,msipotoa huduma kwa kuwajali na kujijali nyinyi wenyewe inaweza kuwa tatizo jingine”,aliongeza Malima.