Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini makubaliano na kampuni ya Tanzania Breweries Plc (TBL) kwa lengo la kuwezesha ufadhili wa mafunzo ya Ufundi wa Zana na Mitambo ya Kilimo (Agro-Mechanics) kwa vijana 300, kupitia mradi uliopewa jina la Ujuzi Kwanza Scholarship.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo, tarehe 28 Oktoba, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore na Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Bi Michelle Kilpin kwenye ofisi za TBL, Ilala jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa hati ya makubaliano iliyosainiwa, makubaliano hayo yanalenga kuwaendeleza vijana wa Kitanzania kwa kuwapatia stadi za vitendo na kuchangia mageuzi ya sekta ya kilimo kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa na rasilimali watu yenye ujuzi stahiki.
Akizungmza kabla ya kusaini makubaliano hayo Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony kasore amesema Mradi wa Ufadhili wa Ujuzi Kwanza, unaendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2050 (Dira 2050), ambayo inatambua kilimo kuwa mojawapo ya sekta tisa zenye uwezo wa kuleta mageuzi makubwa nchini.
“Dira hii inalenga kukibadilisha kilimo kuwa sekta yenye uzalishaji mkubwa, ushindani na endelevu, huku Tanzania ikiimarishwa kuwa kitovu kinachoongoza katika uzalishaji na usambazaji wa chakula katika ukanda huu ifikapo mwaka 2050” amebainisha Kasore.
Kasore ameongeza na kusema kuwa “Ushirikiano huu ni hatua nyingine ya kusonga mbele katika utekelezaji wa Programu ya Ushirikiano kati ya Taasisi za Mafunzo ,Wamiliki wa Viwanda na Waajiri (Training Institutions–Employers Partnership Programme), iliyozinduliwa rasmi mwezi Februari 2026. Aidha, programu hii inachangia katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2024, Toleo la 2023”.
Kasore amebainisha kuwa mradi huo utatekelezwa katika kipindi cha miaka 3 ambapo kwa kila mwaka vijana 100 watapatiwa mafunzo yanayohusu matumizi na matengozo ya zana na mitambo ya kilimo katika vyuo vya VETA vinavyo toa mafunzo hayo ambavyo ni Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma Kihonda (Kihonda RVTSC), Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa cha Manyara (Manyara RVTSC), Chuo cha Ufundi Stadi cha Mpanda (Mpanda VTC), Chuo cha Ufundi Stadi cha Arusha (Arusha VTC) na Chuo cha Ufundi Stadi cha Dakawa (Dakawa VTC).
Ameishukuru TBL kwa kuingia katika ushirikiano huo wenye thamani kubwa na kuongeza kuwa vijana watakaopata ujuzi wataweza kunufaika kwa kuajiriwa au kujiajiri katika sekta ya kilimo.
“Tuna imani kuwa, kupitia ushirikiano huu, VETA itaendelea kuthibitisha uwezo wake wa kutoa mafunzo ya ufundi stadi yenye ubora na umuhimu, yanayozingatia vipaumbele vya taifa na mahitaji ya sekta za uzalishaji na ajira” Ameongeza Kasore
Kwa upande wake Mkurugenze Mtendaji wa TBL Bi. Michelle Kilpin mradi huo umelenga kuleta mabadiliko kubwa na yenye tija katika sekta ya kilimo, kwani kwa miaka mingi wamekuwa wakiwapatia mafunzo wakulima wadogo wa mazao ya mtama, mahindi na shayiri mafunzo ya mbinu bora za kilimo, ushauri wa kitaalamu na teknolojia ya kuongeza mavuno na kwa kuwa VETA imekuwa ikitoa mafunzo katika nyanja hizo wameona ipo haja ya kuunganisha nguvu nakufikia vijana wengi zaidi ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa.
“Sisi kama TBL hatuwekezi tu katika mitambo ya kilimo au mafunzo ya kiufundi tunawekeza kwa watu na kuwapa ujuzi unaohitajika ili kuongeza nguvukazi ya uzalishaji sambamba na kuwa na sekta ya kilimo stahimilivu na endelevu” amesema Bi Kilpin.
Kwa upande wake Neema Temba Mkurugenzi wa mahusiano TBL amesema pamoja na wao kutoa mafunzo kwa wakulima na kupata malighafi kwa ajili ya kuzalisha bidhaa katika kampuni yao wameona ipo haja kuunganisha nguvu na VETA ili kuongeza tija katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.
