Na Silivia Amandius.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Mhe. Devotha Daniel Mburarugaba, ameitaka Serikali kuharakisha ukamilishaji wa miradi ya maji katika Wilaya ya Kyerwa ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo, hususan kwa wanawake wanaotumia muda mwingi kutafuta maji.

Akizungumza kupitia swali bungeni, Mhe. Devotha amehoji lini Serikali itakamilisha miradi ya maji ya Nkwenda, Kaisho na Isingiro ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Maji, Eng. Kundo Mathew, amesema Serikali inatekeleza miradi sita ya maji wilayani Kyerwa, ikiwemo mradi wa Runyinya Chanya wenye thamani ya shilingi bilioni 5.7, ambao umefikia asilimia 92 ya utekelezaji na tayari umeanza kutoa huduma katika vijiji vya Nkwenda, Muulile na Rwabwere.

Amesema mradi huo unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 51,000, huku Serikali ikiendelea kukamilisha hatua ya kwanza ya mradi wa Kaisho–Isingiro wenye thamani ya shilingi bilioni moja, unaohusisha ujenzi wa chanzo cha maji, tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 225,000 na ulazaji wa mabomba.

Aidha, Naibu Waziri amesema miradi ya maji iliyokamilika katika kipindi kilichopita, yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni nne, inaendelea kutoa huduma kwa wananchi, huku miradi inayoendelea kutekelezwa ikiwa na thamani ya jumla ya shilingi bilioni 12.9.

Ameeleza kuwa kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya ya Kyerwa kwa sasa ni asilimia 60, na Serikali inatarajia kukiongeza hadi asilimia 80 baada ya kukamilika kwa miradi inayoendelea, hatua inayolenga kupunguza adha ya maji na kuboresha maisha ya wananchi.