Na Mwandishi Wetu– Dar es Salaam

Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limeipongeza kampuni ya iTrust Finance Limited kwa kuendelea kuleta ubunifu katika soko la mitaji nchini kupitia uzinduzi wa ofa za mifuko mitatu mipya ya uwekezaji inayolenga sekta za fedha, madini na nishati pamoja na mawasiliano na teknolojia.

Mifuko hiyo ni iAfrica Financials ETF, iAfrica Mining & Energy ETF na iAfrica Telco & Tech ETF, ambayo inalenga kuwapa wawekezaji fursa ya kuwekeza katika hisa za kampuni zilizoorodheshwa katika masoko ya hisa ya Afrika, hususan katika sekta zinazochangia maendeleo ya uchumi wa bara hilo.

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Emmanuel Nyalali, Afisa wa Biashara na Maendeleo wa soko hilo, alisema mifuko hiyo inaongeza chaguo la bidhaa za uwekezaji na kupanua fursa kwa wawekezaji wenye malengo na uwezo tofauti wa kifedha.

Alieleza kuwa iAfrica Financials ETF utalenga kampuni zinazotoa huduma za kifedha, zikiwemo benki, kampuni za bima na teknolojia za kifedha, wakati iAfrica Mining & Energy ETF utajikita katika kampuni za madini, mafuta na gesi, umeme pamoja na nishati jadidifu. Kwa upande mwingine, iAfrica Telco & Tech ETF utalenga kampuni za mawasiliano na teknolojia, zikiwemo mitandao ya simu na huduma za kidijitali.

Nyalali alisema mifuko hiyo itasimamiwa kikamilifu na meneja wa uwekezaji atakayechagua na kurekebisha uwekezaji kulingana na malengo ya kila mfuko, kwa lengo la kukuza thamani ya uwekezaji kwa muda mrefu. Kwa mujibu wa nyaraka za ofa, kipande kimoja kinauzwa kwa shilingi 1,000, huku kiwango cha chini cha uwekezaji wa awali kikiwa vipande 100 vyenye thamani ya shilingi 100,000 kwa kila mfuko.

Alisisitiza kuwa uwekezaji wa pamoja unatoa fursa ya kusambaza fedha katika kampuni mbalimbali, lakini wawekezaji wanapaswa kuelewa kuwa thamani ya uwekezaji inaweza kupanda au kushuka kutokana na mabadiliko ya soko na hali za biashara. Aliwataka kusoma nyaraka za ofa, kuelewa gharama na vihatarishi kabla ya kufanya maamuzi ya uwekezaji.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Emmanuel Nyalali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, alisema mamlaka hiyo imeidhinisha nyaraka za ofa na hati za udhamini za mifuko hiyo baada ya iTrust Finance Limited kutimiza matakwa ya kisheria.

Mkama alisema idhini hiyo imetolewa kwa kuzingatia Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania, pamoja na kanuni zinazosimamia uanzishwaji na uendeshaji wa mifuko ya uwekezaji wa pamoja. Alisema hatua hiyo inaonesha umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria katika kuanzisha na kuendesha bidhaa za uwekezaji.

Alieleza kuwa mifuko hiyo itasaidia kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa fursa kwa watu wenye uwezo tofauti wa kifedha kuwekeza kwa pamoja katika masoko ya mitaji. Aliongeza kuwa uwekezaji wa pamoja unaweza kusaidia kupunguza baadhi ya vihatarishi vinavyotokana na kuelekeza fedha katika kampuni moja pekee.

Mkama aliipongeza iTrust Finance Limited pamoja na wadau walioshiriki katika kuanzisha mifuko hiyo, akieleza matumaini yake kuwa itaendeshwa kwa weledi na kutoa manufaa kwa wawekezaji. Pia alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wadau na CMSA katika kuendeleza soko la mitaji na kuongeza ushiriki wa wananchi katika uwekezaji.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa iTrust Finance Limited, Bw. Faiz Arab, alishiriki katika hafla hiyo iliyolenga kutambulisha fursa za uwekezaji kupitia mifuko hiyo mitatu. Uzinduzi wa ofa hizo ni hatua ya kuwapa wawekezaji nafasi ya kujifunza kuhusu mifuko hiyo, kutathmini ufaafu wake na kujiandikisha kununua vipande kabla ya hatua za kuorodheshwa na kuanza biashara katika DSE.

Kwa ujumla, mifuko hiyo inaongeza wigo wa bidhaa za uwekezaji katika soko la mitaji nchini na kuwapa wawekezaji fursa ya kupata uwekezaji katika sekta tofauti za uchumi wa Afrika. DSE imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau husika katika hatua zinazofuata za kuorodheshwa na kuanza kwa biashara ya mifuko hiyo kwa kuzingatia masharti na taratibu zilizowekwa.