Wakaguzi wa Ndani kutoka nchi za Afrika wametakiwa kuzisaidia nchi zao katika kuhakikisha sekta ya mazingira inalindwa na kuhifadhiwa ipasavyo ili rasilimali zake ziendelee kuwanufaisha wananchi.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa Kikundi Kazi cha Ukaguzi wa Mazingira cha Taasisi Kuu za Ukaguzi Barani Afrika (AFROSAI-WGEA) unaofanyika jijini Arusha.
Mkutano huo unawaleta pamoja wakaguzi wakuu na wadau kujadili namna ukaguzi wa mazingira unavyoweza kuimarisha uwajibikaji na maendeleo endelevu ukiwa na kaulimbiu “Ukaguzi kwa Mustakabali Endelevu: Kuendeleza Uchumi wa Buluu, Usalama wa Maji na Udhibiti wa Uchafuzi wa Mazingira kupitia Ushirikiano.”
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa, Dkt. Muyungi aliwataka wakaguzi hao watambue kuwa wao si tu wakaguzi wa hesabu bali pia wana jukumu muhimu la kuhakikisha rasilimali za mazingira zinatumika inavyohitajika.
Aidha, Dkt. Muyungi alieleza kuwa mkutano ni muhimu kwa Tanzania na umekuja wakati muafaka kwa nchi na Bara zima la Afrika kwa ujumla kwani unatoa muelekeo mzuri kwa nchi hizo 33 wanachama katika kushirikiana kujenga ustawi wa sekta ya mazingira.
“Kama tunavyofahamu hivi sasa nchi yetu tumeanza kutekeleza Dira 2025, hivyo suala la ukaguzi wa mazingira tumelipa kipaumbele na ndio maana ile nguzo ya tatu inazungumzia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo ni lazima tutumie utajiri wa rasilimali unaopatikana kutokana na mazingira,” alisema.
Aliongeza kuwa Afrika ina utajiri wa rasilimali kwa mfano ni bara la pili kwa kuwa na eneo kubwa la misitu baada ya ule wa Amazon unaopatikana barani Amerika Kusini (Brazil) akisema Tanzania ina hekta milioni 48.1 zimehifadhiwa sawa na asilimia 33 ya nchi ni misitu.
Hivyo, Dkt. Muyungi alisisitiza umuhimu wa ukaguzi wa mazingira akieleza kuwa sekta mbalimbali za kiuchumi zikiwemo kilimo, mifugo na nishati ambayo inazalishwa kutokana na maji vyanzo vya maji, akieleza kuwa wakaguzi wana mchango katika kuwezesha usimamizi mzuri wa rasilimali hizo.
Kwa upande wake Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CPA Charles Kichere ambaye pia ni Mwenyekiti wa AFROSAI-WGEA alisema agenda kubwa za mkutano huo ni kuzungumzia masuala ya ukaguzi wa hali ya hewa.
Halikadhalika, CPA Kichere aliongeza kuwa wakaguzi wana nafasi ya kuzishauri Serikali za nchi zao namna ya kutunga sera nzuri ambazo zitasaidia kuleta suluhu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mazingira.
Aliongeza kuwa Afrika ina kazi kubwa ya kufanya katika kulinda mazingira hususan katika maeneo ya migodi ambayo inatumia kemikali hasa zebaki katika kutafuta dhahaba, pia ukataji wa miti ambao tayari Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua.

